ترجمة معاني سورة البقرة باللغة السواحلية من كتاب Ali Muhsin Al - Swahili translation

Ali Muhsin Al - Swahili translation

آية رقم 1

Al-Bakarah


Alif Lam Mim.

Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.

Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge, na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia mipaka.

Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale walio kuwa katika zama zao na walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.

Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.

Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale yaliyo tangulizwa na mikono yao; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanao dhulumu.

Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua.

Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na kusujudu.

Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu Yeye tu.

Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.

Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu.

Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.

Ila wale walio tubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.

Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia.

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.

Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.

Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.

Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mkizuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
آية رقم 202

Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.

Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka.

Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Na wanawake walio achwa wangoje peke yao mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu.

Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.

Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.

Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
آية رقم 238

Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
آية رقم 241

Na wanawake walio achwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa wachamngu.

Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.

Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.

Basi Taluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.

MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.

Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.

Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.

Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.

Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.

Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.

Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anakufundisheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:) Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.
تقدم القراءة