ﰡ
Enyi watu! Tahadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri zake na kuepuka makatazo yake, kwani vituko vitakavyotokea pindi kisimamapo Kiyama na mtetemeko mkubwa wa ardhi utakaofanya pambizo zake zipasukepasuke, ni jambo kubwa ambalo hakuna mwenye kulikadiria wala kulifikia vile litakavyokuwa, wala kujua namna yake isipokua Mola wa viumbe wote.
Siku mtakapokiona Kiyama kimesima, mama atamsahau mtoto wake mchanga aliyempa titi lake kunyoya kwa shida iliyomshukia, mwenye mimba ataharibu mimba yake kwa babaiko na akili za watu zitapotea watakuwa ni kama walevi kwa tukio hilo kubwa na babaiko na hali wao si walevi wa pombe, lakini ni ukali wa adhabu ndio uliowapoteza akili zao na hisia zao.
Na baadhi ya vichwa vya ukafiri miongoni mwa watu wanaleta utesi na wanatilia shaka uweza wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa ujinga wao wa kutojua uhakika wa uweza huu na kwa kumfuata kila shetani mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kati ya viongozi wa upotevu.
Mwenyezi Mungu amehukumu na kukadiria juu ya huyu Shetani kwamba yeye ampoteze kila mwenye kumfuata na asimuongoze kwenye ukweli, bali amuandamishe njia ya kupelekea kwenye adhabu ya Jahanamu uliowashwa, ikiwa ni malipo ya kumfuata kwake huyo Shetani.
Enyi watu, mkiwa muna shaka ya kuwa Mwenyzi Mungu atawafufua wafu, basi sisi tumemuumba baba yenu Adam kutokana na mchanga kisha kizazi chake kikazaana kutokana na nutfah, nayo ni manii ambayo mwanamume anayarusha kwenye uzao wa mwnamke, yakageuka kwa uweza wa Mwenyezi Mungu yakawa 'alaqah, nalo ni pande la damu nyekundu iliyo nzito, kisha yakawa mudghah, nacho ni kinofu kidogo cha nyama cha kuweza kutafunika, mara nyingine kikawa kitaumbwa, yaani kiumbike kikamilifu mpaka kifikiye hadi ya kutoka kwa mtoto akiwa hai, na mara nyingine kisiumbike kikamilifu kikatoka kabla ya kutimia, ili tuwafafanulie ukamilifu wa uweza wetu wa kupelekesha miongo ya uumbaji. Na tunakibakisha kwenye zao tunachokitaka, nacho ni kile kinachoendelezwa kuumbwa kwake mpaka wakati wa kuzaliwa kwake na itimie ile miongo ya kuzaliwa wana wa matumboni wakiwa wadogo, wakuwe mpaka wafikie umri wa kuwa na nguvu, nao ni wakati wa ubarobaro na nguvu na kukamilika akili. Na baadhi ya watoto huenda wakafa kabla ya hapo, na baadhi yao wanakuwa mpaka wanafikisha miaka ya ukongwe na udhaifu wa akili, akawa huyu aliyezeeka hajui kitu alichokuwa akikijua kabla ya hapo. Na utaiyona ardhi ni kavu, imekufa haina mimea yoyote, tuyateremshapo maji juu yake, inatikisika kwa mimea ikawa inafunguka, inachepuza, inanyanyuka na kuongezeka kwa kutosheka na maji na ikaotesha kila aina ya mimea mizuri yenye kuwafurahisha wenye kuangalia.
Hayo yaliyotangulia kutajwa, miongoni mwa alama za uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ndani yake pana dalili ya kukata kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika, Ndiye Mola Mwenye kuabudiwa kwa haki Ambaye hakuna anayefaa kuabudiwa isipokuwa Yeye, na Yeye Ndiye Mwenye kuwahuisha wafu, na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na kwamba wakati wa ufufuzi ni wenye kuja, hilo halina shaka, na kwamba Mwenyezi Mungu Atawafufua wafu kutoka makaburini mwao ili Awahesabu na Awalipe.
Miongoni mwa makafiri kuna wenye kujadili kwa njia ya ubatilifu kuhusu Mwenyezi Mungu na kuhusu kumpwekesha Yeye na kuhusu kumteua Kwake Mitume wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuhusu kuteremsha Kwake Qur’ani. Kujadili huko ni bila ya ujuzi, ufafanuzi wala kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu chenye ushahidi na hoja iliyo wazi,
hali akiipotoa shingo yake kwa kiburi na akiupa mgongo ukweli, ili awazuie wengine wasiingie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu. Basi huyo atapata hizaya ulimwenguni kwa kuangamia na mambo yao kufedheheka; na Siku ya Kiyama tutamchoma kwa Moto.
Na ataambiwa, «Adhabu hiyo ni kwa sababu ya maasia uliyoyafanya na makosa uliyoyachuma, na Mwenyezi Mungu Hamuadhibu yoyote pasi na dhambi.»
Miongoni mwa watu kuna anayeingia kwenye Uislamu kwa udhaifu na shaka, akawa anamuabudu Mwenyezi Mungu juu ya shaka na ukosefu wa uamuzi, ni kama yule anayesimama kwenye ukingo wa jabali au ukuta, hawi thabiti katika kusimama kwake, huifungamanisha Imani yake na ulimwengu wake: akiishi katika hali ya afya na ukunjufu huendelea kwenye ibada yake, na akipatikana na mitihani ya tabu na shida huyanasibisha hayo na Dini yake, na kwa hivyo huiacha. Ni kama yule anayegeuka kwa uso wake baada ya kulingana sawa, hivyo basi akapata hasara ya ulimwengu, kwani kukufuru kwake hakugeuzi chochote alichokadiriwa katika ulimwengu wake, na akapata hasara ya Akhera kwa kuingia Motoni, na hiyo ni hasara inayoonekana waziwazi.
Huyo aliyepata hasara anakiabudu kitu, badala ya Mwenyezi Mungu, kisichomdhuru lau akikiwacha wala kumnufaisha akikiabudu. Huko ndiko kupotea kulioko mbali na haki.
Anamubudu ambaye madhara yake ya hakika yako karibu zaidi kuliko manufaa yake, ni ubaya ulioje wa muabudiwa huyo kuwa ni muokozi na ni ubaya uilioje wake kuwa ni wakutangamana naye.
Hakika Mwenyezi Mungu Atawatia, wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakajikita katika hiyo Imani na wakafanaya mema, kwenye mabustani ya Pepo ambayo inapata mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Hakika Mwenyezi Mungu Anafanya Analolitaka la kuwapa malipo mazuri wenye kumtii kwa ukarimu Wake na kuwatesa wenye kumuasi kwa uadilifu Wake.
Yoyote yule anayeitakidi kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hatamsaidia Mtume Wake kwa kumpa ushindi ulimwenguni kwa kuipa nguvu Dini yake na huko Akhera kumtukuza daraja yake na kumuadhibu aliyemkanusha, basi anyoshe kamba aifunge kwenye sakafu ya nyumba yake kisha ajitie kitanzi kisha aikate hiyo kamba, kisha aangalie iwapo hilo litamuondolea hasira alizonazo ndani ya nafsi yake. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumnusuru Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, hapana budi.
Na kama Alivyosimamisha Mwenyezi Mungu hoja, miongoni mwa dalili za uweza Wake, juu ya makafiri kuhusu ufufuzi, vilevile Aliiteremsha Qur’ani, ambayo aya zake ziko wazi katika matamshi yake na maana yake na ambayo kwayo Mwenyezi Mungu Anamuongoza anayemtaka aongoke. Kwani hakuna Mwenye kuongoa isipokuwa Yeye.
Hakika wale waliomumini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na Mayahudi na Sābiūn (watu waliobaki kwenye maumbile yao na hawana dini wanayoifuata) na Wanaswara na Majūs (wnaoabudu moto) na wale walioashirikisha (wanaoabudu masanamu), Mwenyezi Mungu Atapambanua baina yao wote, Siku ya Kiyama, Awatie Waumini Peponi na Awatie makafiri Motoni, Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Shahidi, Anayashuhudia matendo yote ya waja, Anayadhibiti na Anayahifadhi, Na Atamlipa kila mtu kile anachostahili, malipo yanayolingana na matendo waliokuwa wakiyafanya.
Je hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, wanamsujudia Yeye, katika hali ya kunyenyekea na kufuata amri, Malaika walioko mbinguni, viumbe walioko ardhini, jua, mwezi, majabali, miti na wanyama? Na wanamsujudia Mwenyezi Mungu, kwa kutii na kwa hiari, watu wengi, nao ni Waumini. Na kuna watu wengi imepasa adhabu juu yao, na kwa hivyo wao ni watwevu. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemtweza hakuna yoyote wa kumtukuza. Hakika Mwenyezi Mungu Anafanya kwa viumbe vyake Atakalo kuambatana na hekima Yake.
Haya ni mapote mawili ya watu, wametafautiana kuhusu Mola wao: watu wa Imani na watu wa ukafiri, kila mmoja anadai kuwa yeye yuko kwenye usawa. Wale waliokufuru watazungukwa na adhabu yenye sura ya nguo za Moto walizopatiwa wazivae, zitaichoma miili yao na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yaliyofikia upeo wa ukali,
hapo yateremke ndani ya matumbo yao na viyayuke vilivyomo ndani yake mpaka yapenyeze kwenye ngozi zao yazichome na zitoke na kuanguka.
Na Malaika watawapiga vichwa vyao kwa nyundo za chuma.
Na kila wakijaribu kutoka Motoni, kwa sababu ya makero na mateso walionayo, watarudishwa adhabuni na wataambiwa, «Onjeni adhabu ya Moto unaochoma.»
Hakika Mwenyezi Mungu Atawatia watu wa Imani na matendo mema kwenye mabustani ya Pepo ambayo starehe yake ni ya daima, inapita mito chini ya miti yake, watapambwa humo kwa makuku ya dhahabu na kwa lulu; na nguo zao za kawaida Peponi ni hariri kwa wanawake na kwa wanaume.
Kwa hakika, Mwenyezi Mungu Aliwaongoza ulimwenguni kwenye neno zuri: tamshi la kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumshukuru na kumsifu, na huko Akhera wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mwisho mwema, kama vile Alivyowaongoza kabla ya hapo kufuata njia ya Uislamu inayosifiwa inayofikisha Peponi.
Hakika wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na wakayakanusha yale ambayo alikuja nayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakawazuia wengine kuingia kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu, wakamzuia Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pamoja na waumini katika mwaka wa Ḥudaybiyah wasiingie Msikiti wa Ḥarām tulioufanya ni wa Waumini wote, wanaokaa hapo na wanaokuja kuukusudia, hao watapata adhabu kali yenye kuumiza. Na yoyote anayetaka, ndani ya Msikiti wa Ḥarām, kuenda kombo na haki kwa njia ya udhalimu na akamuasi Mwenezi Mungu humo ndani, basi tutamuonjesha adhabu kali yenye kuumiza.
Taja, ewe Nabii, pindi tulipomuelezea Ibrāhīm, amani imshukiye, mahali pa Nyumba, tukamtayarishia yeye mahali hapo, na palikua hapajulikani. Na tulimuamrisha aijengi juu ya misingi ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha na aisafishe na ukafiri na mambo ya uzushi na uchafu, ili iwe ni mahali pakunjufu kwa wenye kuizunguka kwa kutufu na wenye kuswali hapo.
na uwajulishe watu, ewe Ibrāhīm, uwajibu wa Hija juu yao, watakujia kwa kila namna zao, wakiwa wanatembea kwa miguu na wakiwa wanapanda, miongoni mwa ngamia, kila aliyeambata matumbo kwa kutembea na kufanya kazi na sio kwa udhaifu. Watakuja kutoka njia ya mbali,
ili kuyahudhuria yenye kuwafaa ya kusamehewa dhambi zao, kulipwa thawabu za utekelezaji wa ibada yao ya Hija na utiifu wao, kujipatia mapato katika biashara zao na mengine yasiokuwa hayo. Na ili wataje jina la Mwenyezi Mungu kwa kuchinja wanyama ambao kwao wanajisongeza karibu na Mwenyezi Mungu, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, katika siku maalumu: nazo ni siku ya kumi ya Mfungotatu na siku tatu baada yake, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake. Na wao wameamrishwa kwa kupendekezewa kula katika vichinjwa hivi na kumlisha kutokana nazo masikini ambaye umasikini wake umembana.
Kisha wale mahujaji wakamilishe matendo ya ibada yaliyosalia ya kujifungua na kutoka kwenye kifungo cha ibada yao ya Hija, nako ni kwa kuondoa uchafu uliokusanyika kwenye miili yao, kukata kucha zao na kunyoa nywele zao, na watekeleze yale waliyojilazimsha nafsi zao ya kuhiji na kufanya Umra na kuchinja wanyama wa tunu, na waitufu kwa kuizunguka Nyumba huru ya kale ambayo Mwenyezi Mungu Ameikomboa isitawaliwe kimabavu na watu wasioijali, nayo ni Alkaba.
Hiyo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya kuondoa uchafu, kutekeleza nadhiri na kuitufu Nyumba ndiyo Aliyoyapasisha Mwenyezi Mungu, basi yatukuzeni. Na yoyote mwenye kuyatukuza Aliyoyatakasa Mwenyezi Mungu, na miongoni mwayo ni matendo Aliyoyawekea ibada ya Hija kwa kuyatekeleza kikamilifu kwa kumtakasia Mwenyezi Mungu, basi hilo ni bora zaidi kwake, ulimwenguni na Akhera. Na Mwenyezi Mungu Amewahalalishia nyinyi kula wanyama-howa isipokuwa kile Alichokiharamisha kwenu katika kile mnachosomewa ndani ya Qur’ani miongoni mwa mizoga na mengineyo, basi kiepukeni. Katika hili pana kubatilisha kile ambacho Waarabu walikuwa wakikiharamisha cha baadhi ya wanyama-howa. Na jiekeni mbali na uchafu ambao ni masanamu na urongo wa kumzulia Mwenyezi Mungu.
Hali ya kulingana sawa kwa Mwenyezi Mungu juu ya kumtakasia matendo, kumuelekea Yeye kwa kumuabudu Yeye Peke Yake na kumpwekesha kwa utiifu na kumuepuka kila asiyekuwa Yeye kwa kukataa ushirikina, kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu chochote, mfano wake- katika kuwa mbali kwake na uongofu na katika kuangamia kwake na kuanguka kwake kutoka kwenye kilele cha Imani hadi kwenye shimo la ukafiri na wakawa Mashetani wanamnyakuwa kutoka kila upande - ni kama mfano wa mtu aliyeanguka kutoka mbinguni, ima ndege watamnyakuwa na kumkatakata viungo vyake au kimbunga kikali cha upepo kitamchukua kimtupe mahali mbali sana.
Hayo ndiyo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya kumpwekesha na kumtakasia ibada. Na yoyote mwenye kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na akayatukuza mambo makubwa ya Dini, na miongoni mwayo ni matendo ya Hija na sehemu zake na wanyama wanaochinjwa huko, kwa kuchagua walio wazuri na walio wanono, basi kutukuza huko ni katika vitendo vya wenye nyoyo zenye kusifika kwa kumcha Mwenyezi Mungu na kumuogopa.
Muna nyinyi, katika wanyama hawa wa kutolewa tunu, manufaa ya nyinyi kunufaika nayo miongoni mwa sufi, maziwa, kipando na megineyo ambayo hayawadhuru hao wanyama mpaka wakati wa kuchinjwa huko kwenye Nyumba ya kale, nako ni eneo lote takatifu.
Na kila kundi lenye kuamini lililotangulia, tumelifanyia mambo ya ibada ya kuchinja na kumwaga damu, hayo ni kwa ajili wapate kutaja jina la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wakati wa kuchinja kile tulichowaruzuku cha hawa wanyama-howa na wamshukuru. Basi Mola wenu, enyi watu, ni Mola Mmoja, Yeye ni Mwemyezi Mungu. Hivyo basi iandameni amri Yake na amri ya Mtume Wake. Na uuwape bishara njema, ewe Mtume, wale wanyenyekevu waliosalimu amri kwa Mola wao, kwamba watapata kheri mbili: ya ulimenguni nay a Akhera.
Wanyenyekevu hawa wenye kujinyongesha (kwa Mwenyezi Mungu) miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao Atajwapo Mwenyezi Mungu Peke Yake, wanaiyogopa adhabu Yake na wanakuwa na hadhari wasimuasi, na wakipatikana na shida na matatizo, wanasubiri juu ya hayo wakiwa na matumaini kupata malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, wanatekeleza Swala kikamilifu, na wao pamoja na hayo wanatoa, katika kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, katika mambo yanayowapasa ya Zaka, matumizi ya watoto na kila ambaye matumizi yake yanawalazimu, katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika matumizi yanayopendekezwa yasio ya lazima.
Na tumewafanyia nyinyi kule kuchinja ngamia ni miongoni mwa alama za Dini na mambo yake makubwa. Ili mpate kujisongeza karibu na Mwenyezi Mungu kwayo. Katika hao nyinyi, enyi wenye kujisongeza karibu naye, muna kheri katika manufaa yake ya kula, kutoa sadaka na kupata malipo ya thawabu. Basi semeni mnapowachinja, «Bismillāh» (kwa jina la Mwenyezi Mungu). Na ngamia huchinjwa akiwa amesimama, miguu yake mitatu imepangwa na mmoja umefungwa, basi akianguka kwa mbavu zake, huwa amekuwa halali kumla. Wale waliomchinja kwa ajili ya ibada na wale kitu katika mnyama huyo na wamlishe kutokana naye aliyekinai, naye ni muhitaji asiyeomba kwa kujihifadhi, na muhitaji anayeomba kumaliza haja yake. Hivi ndivyo Alivyowadhalilishia Mwenyezi Mungu ngamia, huenda mukamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwadhalilishia.
Hazitamfikia Mwenyezi Mungu nyama za vichinjwa hivyi wala damu zake kitu chochote, kitakachomfikia Yeye ni kule kumtakasia kwenu katika hivyo na kuwa lengo lake ni radhi za Mwenyezi Mungu Peke Yake. Hivyo basi Amewadhalilishia nyinyi, enyi wenye kujikurubisha, ili mumtukuze Mwenyezi Mungu na mumshukuru kwa kuwaongoza kwenye haki, kwani Yeye Anastahiki hilo. Na uwape bishara njema, ewe Nabii, wenye kufanya wema kwa kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake na kuwafanyia wema viumbe vyake, kupata kila lema na kufaulu.
Hakika Mwenyezi Mungu Anawalinda Waumini na uadui wa makafiri na vitimbi vya waovu, kwani Yeye, Aliyeshinda na kutukuka, Hampendi kila mwingi wa hiana wa amana ya Mola wake, mwingi wa kukanusha neem Zake.
Waislamu, mwanzo wao, walikuwa wamekatazwa kupigana na makafiri, wameamrishwa kuvumilia maudhi yao. Maudhi ya washirikina yalipofikia upeo wake na Mtume akatoka Makkah hali ya kugura kwenda Madina na Uislamu ukawa na nguvu, Mwenyezi Mungu Aliwaruhusu Waislamu kupigana kwa sababu hiyo ya maonevu yaliyowashukia na uadui. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwanusuru na kuwadhalilisha maadui wao.
Wale ambao walilazimishwa kutoka majumbani mwao, si kwa lolote isipokuwa ni kwa kuwa wamesilimu na wamesema, «Mola wetu ni Mwenyezi Mngu Peke Yake.» Na lau si mpango Aliouiweka Mwenyezi Mungu wa kuondoa maonevu ambayo kwayo wananufaika watu wa dini zote zilizoteremshwa na kuurudisha ubatilifu kwa kuruhusu kupigana, haki ingalishindwa katika kila ummah, ardhi ingaliharibiwa, sehemu za ibada zingalivunjwa, miongoni mwa mindule ya watawa, makanisa ya Wanaswara, majumba ya ibada ya Mayahudi na misikiti ya Waislamu ambayo Wanaswali ndani yake, na wanamtaja Mwenyezi Mungu humo kwa wingi. Na mwenye kufanya bidii kuitetea Dini ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Atamnusuru juu ya adui yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa, ni Mshindi Asiyefikiwa, Amewatendesha nguvu viumbe na Amezishika paa za nyuso zao.
Wale tuliowaahidi kuwa tutawanusuru ndio wale tukiwapa utulivu kwenye ardhi na kuwatawalisha humo kwa kuwapa ushindi juu ya adui wao, wanasimamisha Swala kwa kuiitekeleza kwa nyakati zake kwa namna zake, wanatoa Zaka za mali zao kuwapa wastahiki wake, wanaamrisha kila ambalo Mwenyezi Mungu Ameliamrisha la haki Zake na haki za waja Wake na wanakataza kila ambalo Mwenyezi Mungu Amelikataza na Mtume Wake. Na ni wa Mwenyezi Mungu Peke Yake mwisho wa mambo yote, na mwisho mwema ni wa uchamungu.
Na wakikukanusha watu wako, ewe Mtume, basi wamewatangulia wao katika kukanusha Mitume wao watu wa Nūḥ,' Ād, Thamūd
na watu wa Ibrāhīm na watu wa Lūṭ
na watu wa Madyan waliomkanusha Shu'ayb na pia Fir'awn na watu wake walimkanusha Mūsā. Sikuwaharakishia ummah hao mateso, bali niliwapa muda kisha kila mmoja wa hao niliupatiliza kwa adhabu. Ilikuwaje vile nilivyowakataza wao ukafiri wao na ukanushaji wao na nilivyowabadilishia neema waliokuwa nayo kwa adhabu na maangamivu?
Ni miji mingi iliyojidhulumu kwa ukafiri wake, tuliwaangamiza watu wake, nyumba zao zikavunjwa zikawa ziko tupu hazina wakazi wake, visima vyake vikawa havichotwi maji na majumba yake ya fahari yaliyo marefu yaliyopambwa hayakuwakinga watu wake na adhabu kali.
Si watembee hao wakanushaji wa Makureshi kwenye ardhi wajionee athari za walioangamizwa, wafikirie kwa akili zao na wazingatie na wasikie habari zao kusikia kwa mazingatio wapate kuwaidhika? Kwani upofu si upofu wa macho, hakika ya upofu wenye kuangamiza ni upofu wa busara wa kutoijua haki na kutozingatia.
Na makafiri wa Kikureshi, kwaujinga wao, wanakuharakisha, ewe Mtme, uwaletee adhabu ambayo uliwaonya nayo baada ya kuwa wakakamavu juu ya ukafiri. Mwenyezi Mungu Hataenda kinyume na ahadi yake ya adhabu aliyowaonya nayo, haina budi kutuka. Na hapa duniani Aliwaharakishia hiyo, siku ya vita vya Badr. Na siku moja miongoni mwa siku mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama miaka alfu moja mnazozihesbu katika miaka duniani.
Kuna miji mingi ilikuwa kwenye udhalimu, kwa ukakamavu wa watu wake juu ya ukafiri, nikawapa muda , na sikuwaharakishia adhabu na kwa hivyo wakaghurika, kisha nikawachukuwa kwa kuwaadhibu katika hii dunia, na ni kwangu ndio marejeo yao baada ya kuangamia kwao nitawapa adhabu wanayostahili
Sema, ewe Mtume, «Enyi watu! Mimi si kuwa isipokuwa ni muonyaji kwenu mwenye kumfikishia Mwenyezi Mungu ujumbe Wake.
Basi wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na imani hiyo ikajikita kwenye nyoyo zao na wakafanya matendo mema, watapata msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Mola wao na sitara ya kufinika matendo ya uasi yaliyotokana na wao na riziki nzuri isiyokatika nayo ni Pepo.
Na wale wenye kujitahidi kufanya vitimbi ili kuzitangua aya za Qur’ani kwa kuzikanusha hali ya kuwa ni watesi na washindani, basi hao ndio watu wa Moto wenye kuwaka, wataungia na watasalia humo milele.»
Na hatukuwatumiliza kabla yako wewe, ewe Mtume, Mtume yoyote wala Nabii isipokuwa asomapo kitabu cha Mwenyezi mungu, Shetani anatia katika kisomo chake wasiwasi na tashwishi, ili kuwazuilia watu kufuata kile anachokisoma. Lakini Mwenyezi Mungu Anatangua vitimbi vya Shetanai, Anauondoa ushawishi wake na Anathibitisha aya Zake zilizo wazi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyokuwa na yatakayokuwa, hakuna kinachofichika Kwake chochote, ni Mwingi wa hekima katika makadirio Yake na amri Zake.
Na hakikua kitendo hiki kutoka kwa Shetani isipokuwa Mwenyezi Mungu Akifanye ni mtihani kwa wale ambao ndani ya nyoyo zao muna shaka na unafiki na kwa wale washirikina washupavu wa nyoyo ambao haliathiri kwao kemeo lolote. Na kwa hakika, madhalimu miongoni mwa hawa na wale wako kwenye uadui mkubwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na upingaji haki ulio mbali na usawa.
Na ili wapate kujua wenye elimu ambao wanapambanua, kwa ujuzi wao, baina ya ukweli na urongo kwamba Qur’ani tukufu ndio haki iliyoteremka juu yako, ewe Mtume, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, haina udanganyifu ndani yake na hakuna njia yoyote ya Shetani kuifikia, na kwa hiyo imani yao inaongezeka na nyoyo zao zinainyenyekea. Na hakika ya Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaongoa wale walioiamini na wakamuamini Mtume Wake kwenye njia ya haki iliyo wazi, nayo ni Uislamu, na Atawaokoa kwayo na upotevu.
Na hawataacha makafiri wenye kukanusha kuendelea kuwa kwenye shaka juu ya Qur’ani uliokuja nayo mpaka Kiyama kiwajie kwa ghafula na hali wao wako juu ya ukanushaji wao, au iwajie wao adhabu ya Siku isiyokuwa na wema ndani yake, nayo ni Siku ya kiyama.
Ufalume na mamlaka katika Siku hii ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ataamua baina ya Waumini na makafiri. Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, ni zao wao starehe za daima kwenye mabustani ya Pepo.
Na wale walioukataa upwekwe wa Mwenyezi Mungu, wakawakanusha Mitume Wake na wakazipinga aya za Qur’ani, basi hao watapata adhabu yenye kuwafanya wanyonge na kuwatweza ndani ya moto wa Jahanamu.
Na wale waliyotoka majumbani mwao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kuinusuru Dini Yake, yoyote kati yao atakayeuawa akiwa katika hali ya kupigana na makafiri, na yoyote kati yao atakayekufa bila kupigana, Mwenyezi Mungu Atawaruzuku Pepo na starehe zake zisizokatika wala kuondoka. Na kwa hakika, Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku.
Atawatia Mola wao tena Atawatia mahali pa kuingia ambapo watapapenda, napo ni Peponi. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu Anamjua sana yule anayetoka katika njia Yake na mwenye kutoka kwa ajili ya ulimwengu, ni Mpole kwa wale waliomuasi hawafanyii haraka kuwatesa.
Hilo ni jambo tulilokusimulia la kuwatia Peponi waliogura(katika njia ya Mwenyezi Mungu), na mwenye kufanyiwa uadui na kuonewa basi yeye ameruhusiwa kupambana na huyo mhalifu kwa kitendo kama chake, na atakuwa hana makosa. Na akirudi yule mhalifu kumuonea na akafanya udhalimu, basi Mwenyezi Mungu Atampa ushindi yule mdhulumiwa aliyeonewa, kwani haifai afanyiwe uadui kwa kuwa amejilipizia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehefu ni Mwingi wa kughofiria, Anasamehe dhambi za wenye kukosea, hawafanyii haraka kuwatesa na anazifinika dhambi zao.
Huyo Aliyewaekea hukumu hizo za uadilifu Ndiye wa kweli, na Yeye Ndiye Muweza waAlitakalo. Na katika uweza Wake ni kwamba Yeye Anaziingiza saa za usiku zipunguazo kwenye saa za mchana, na anaziingiza saa za mchana zipunguazo kwenye saa za usiku na kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila sauti, ni Muoni wa kila kitendo, hakifichiki kitu chochote Kwake.
Hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki Ambaye hapana yoyote Anayepasa aabudiwe isipokuwa Yeye na kwamba vile wanavyoviabudu washirikina miongoni mwa masanamu na waungu-bandia wanaodaiwa kufanana na Yeye ndio batili wasionufaisha wala kudhuru, na kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliye juu ya viumbe vyake kwa dhati, cheo na utendeshaji nguvu, Ndiye Aliyejiepusha na wanaodaiwa kufanana na Yeye na kuwa wendani Wake, Aliye Mkuu katika dhati Yake, majina Yake na sifa Zake. Yeye ni Mkubwa kuliko kila kitu.
Je, huoni, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu Ameteremsha mvua kutoka mbinguni, ardhi ikawa kijani kwa mimea iliyomea? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma na upole kwa waja Wake kwa kuitoa mimea kutoka ardhini kwa maji hayo, ni mtambuzi wa mambo yanayowafaa.
Ni vya Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, vilivyoko ardhini na mbinguni, kwa kuviumba, kuvimiliki na kuwa chini ya usimamizi wake, kila kimoja kati ya hizo kinahitajia uendeshaji Wake na maneemesho Yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Ndie Aliye Mkwasi ambaye Hahitajii kitu chochote, Anayeshukuriwa kwa kila namna.
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewadhalilishia vilivyoko ardhini miongoni mwa vitu vitambaavyo na wanyama na nafaka na matunda na vitu visivyo na roho, kwa ajili ya kipando chenu, chakula chenu na manufaa yenu, kama Alivyowadhalilishia mashua zinazotembea baharini kwa uweza Wake na amri Yake, ziwabebe nyinyi na vyombo vyenu ziwafikishe kwenye miji na sehemu mzitakazo na kwamba Yeye Ndiye Anayeizuia mbingu na kuitunza, ili isianguke juu ya ardhi ikawaangamiza walioko juu yake isipokuwa kwa idhini Yake, Aliyetakasika na kila sifa za upungufu, kuwa hilo lifanyike, ili Awarehemu watu rehema kunjufu katika mambo yao ya hivi sasa hapa duniani na ya baadaye kesho Akhera? Na miongoni mwa rehema Zake ni vitu hivi Alivowadhalilishia na vinginevyo kwa fadhila Zake juu yao.
Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyewapa uhai kwa kuwafanya mupatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako, kisha Atawafisha umri wenu ukomapo, kisha Atawahuisha kwa kuwafufua ili Awahesabu kwa matendo yenu. Hakika mwanadamu ni mwingi wa kukataa alama zenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu na upweke Wake.
Kila watu miongoni mwa jinsi za watu waliopita tumewaekea sheria na ibada tuliowaamrisha wao kwazo, na wao ni wenye kuzitumia, basi wasikufanyie ushindani, ewe Mtume, hao washirikina wa Kikureshi kuhusu Sheria yako na yale Aliyokuamrisha Mwenyezi Mungu katika matendo ya Hija na aina zote za ibada. Na ulinganie kwenye kumpwekesha Mola wako na kumtakasia ibada na kufuata amri Yake. Hakika wewe uko kwenye Dini iliyolingana sawa, isiyokuwa na mapindi.
Na wakishikilia kujadiliana na wewe kwa njia ya ubatilifu kuhusu yale unayowalingania nayo, usijadiliane na wao, bali waambie, «Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi wa mnayoyafanya ya ukafiri na kukanusha,» kwani wao wanafanya inadi na kiburi.
Mwenyezi Mungu Atahukumu kati ya Waislamu na makafiri Siku Ya Kiyama katika tafauti zao kuhusu dini. Katika aya hii pana adabu nzuri ya kuwarudi wanaofanya mjadala kwa njia ya ujeuri na kiburi.
Je, hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu anavijua vilivyomo mbinguni na ardhini ujuzi kamili Aliouthibitisha katika Ubao Uliohifadhiwa? Ujuzi huo ni jambo sahali kwa Mwenyezi Mungu Ambaye hakuna kitu kinachomshinda.
Na makafiri wa Kikureshi wanashikilia kumshirikisha Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa ubatilifu wa waliyonayo uko waziwazi. Wao wanawaabudu waungu ambao haukuteremka, kwenye kitabu chochote miongoni mwa vitabu vya Mwenyezi Mungu, ushahidi kuwa wao wanafaa kufanyiwa ibada, na wao (hao waungu) hawajui chochote kuhusu yale waliyoyazua (hao makafiri) na kumsingizia Mwenyezi Mungu, hakika hilo ni jambo ambalo kwalo wamewafuata baba zao bila dalili yoyote. Basi kitakapokuja kipindi cha kuhesabiwa huko Akhera, hawa washirikina hawatakuwa na msaidizi mwenye kuwanusuru au kuwakinga na adhabu.
Na pindi zinaposomwa kwa washirikina aya za Qur’ani zilizo wazi, utauona uchukivu waziwazi kwenye nyuso zao, wanakaribia kuwapiga Waumini wanaowalingania kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuwasomea aya Zake. Basi waambie, ewe Mtume, «je, si niwape habari ya kitu chenye kuchukiza zaidi kwenu kuliko kuisikia haki na kuwaona walinganizi wake? Ni Moto ambao Mwenyezi Mungu Ameutayarisha kwa makafiri huko Akhera. Na mahali pabaya zaidi pa mtu kuishia ni hapo.»
Enyi watu! Kumepigwa mfano, usikilizeni na muuzingatie: Kwa hakika, masanamu na wanaodaiwa kufanana na Mwenyezi Mungu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoweza lau wakikusanya kuumba nzi mmoja, basi itakuaje kuumba kikubwa zaidi? Wala hawawezi kukirudisha kitu alichokinyakua nzi kutoka kwao, Je kuna kuelemewa zaidi kuliko huko? Vyote viwili pamoja ni vinyonge: amedhoofika mtaka kurudisha kitu kilichochukuliwa na nzi kutoka kwake, naye ni yule muabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, na pia amedhoofika mtakwa, naye ni nzi. Basi vipi hawa masanamu na wanaofanywa kuwa wanafanana na Mwenyezi Mungu watafanywa ni waungu, ilhali wao wako kwenye udhaifu huu?
Hawa washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu vile Anavyostahiki kutukuzwa, kwa kuwa wao wamemfanya kuwa Ana washirika, na hali Yeye Ndiye Mwenye nguvu Aliyeumba kila kitu, Ndiye Mshindi Asiyeshindwa.
Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anateua, miongoni mwa Malaika, wajumbe kuwatuma kwa Manabii Wake, na Anateua kutokana na watu, wajumbe wakufikisha jumbe Zake kwa viumbe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja Wake, Mwenye kuviona vitu vyote na yule anayemteua kwa utume miongoni mwa viumbe Wake. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake,
Anayajua yaliyo mbele ya Malaika wake na Mitume Wake kabla hajawaumba, na Anayajua yenye kuwa baada ya kutoweka kwao. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, yanarejea mambo yote.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, rukuuni na sujuduni katika Swala zenu na muabuduni Mola wenu, Peke Yake, Asiye na mshirika, na fanyeni wema ili mufuzu,
na zipigeni jihadi nafsi zenu, na simameni, kisimamo kikamilifu, kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na waiteni viumbe kwenye njia Yake, na piganeni jihadi kwa mali zenu, ndimi zenu na nafsi zenu, hali ya kumtakasia nia Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa hayo, hali ya kuzisalimisha Kwake nyoyo zenu na viungo vyenu. Yeye Amewateua muibebe hii Dini. Na Amewapa neema kwa kuifanya Sheria Yake kuwa sahali, haina dhiki wala mikazo katika Amri zake na hukumu zake kama vile ilivyokuwa kwa baadhi ya ummah kabla yenu. Mila hii yenye usahali ndio Mila ya baba yenu Ibrāhīm. Na Mwenyezi Mungu Amewaita nyinyi Waislamu tangu nyuma kwenye Vitabu vilivyoteremshwa vilivyotangulia na katika hii Qur’ani. Na Amewahusu nyinyi kwa chaguo hili, ili mwisho wa Mitume, Mhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, awe shahidi wenu kuwa amewafikishia ujumbe wa Mola wake, na ili muwe ni mashahidi wa ummah wengine kuwa Mitume wao waliwafikishia kwa habari mlizopewa na Mwenyezi Mungu katika Kitabu Chake. Basi jibidiisheni kujua thamani ya neema hii mupate kuishukuru, na mujilazimishe kufuata maamrisho ya Dini ya Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza Swala kwa nguzo zake na sheruti zake na kutoa Zaka za faradhi, na muingie kwenye himaya ya Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, na mumtegemee Yeye, kwani yeye Ndiye Mbora wa kutegemewa kwa mwenye kumtegemea na ni Mbora wa kunusuru kwa anayeomba nusura Yake.