ترجمة سورة الزمر

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الزمر باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Kuteremshwa Qur’ani, Hakika ni kwamba, ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mshindi katika uweza Wake na utesaji Wake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na hukumu Zake.
Kwa hakika sisi tumekuteremshia, ewe Mtume, Qur’ani inayoamuru haki na uadilifu. Basi muabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na umtakasie mambo yote ya Dini yako.
Jua utanabahi kwamba ni haki ya Mwenyezi Mungu, Peke Yake, kutiiwa utiifu uliyotimia uliosalimika na ushirikina. Na wale wanaomshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu wakawafanya wasiokuwa Yeye kuwa ni wategemewa, wanasema, «Hatuwaabudu waungu hawa pamoja na Mwenyezi Mungu isipokuwa wapate kutuombea kwa Mwenyezi Mungu na ili watukurubishe daraja Kwake.» Hivyo basi wakakufuru, kwani ibada na uombezi ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Hakika Mwenyezi Mungu Atawapambanua, Siku ya Kiyama, baina ya Waumini wenye ikhlasi na wale wenye kumshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, katika yale waliokuwa wanatafautiana juu yake kuhusu vile walivyoabudu. Hapo amlipe kila mmoja kwa anachostahiki. Hakika Mwenyezi Mungu hawaelekezi kuongoka kwenye njia iliyonyoka wale wenye kumzulia urongo Mwenyezi Mungu, wenye kuzikanusha aya Zake na hoja Zake.
Lau Angalitaka Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto, Angalichagua, miongoni mwa viumbe Vyake, Anachotaka. Ameepukana Mwenyezi Mungu na kutakasika na kuwa na mtoto! Hakika Yeye ni Mmoja Aliye Pekee na kupwekeka, Mwenye kutegemewa kwa kila haja, Mwenye kutendesha nguvu ambaye Amewalazimisha viumbe kwa uweza Wake, basi kila kitu kinamdhalilikia Yeye na kumnyenyekea.
Ameumba Mwenyezi Mungu mbingu na ardhi na viliyomo ndani yake, Anauleta usiku na kuuondoa mchana, na Anauleta mchana na kuuondoa usiku. Na Amelidhalilisha jua na mwezi ili manufaa ya waja yapangike. Kila mojawapo ya hivi viwili vinatembea kwenye sehemu yake ya kuzunguka mpaka kipindi cha kusimama Kiyama. Jua utanabahi, hakika Mwenyezi Mungu Aliyefanya matendo haya na Akawapa waja Wake neema hizi, Ndiye Mshindi juu ya viumbe Vyake, ni Mwingi wa kusamehe dhambi zao.
Amewaumba nyinyi Mola wenu, enyi watu, kutokana na Ādam, na Akamuumba kutokana naye mke wake, na Akawaumbia, katika wanyama-hoa, aina nane za kiume na kike, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi. Anawaumba nyinyi matumboni mwa mama zenu, muongo baada ya muongo wa uumbaji ndani ya magiza ya tumbo, kizazi na kifuko. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyeumba vitu hivi, Mola wenu Aliyepwekeka kwa ufalme na Aliye Mmoja katika uungu, Anayestahiki kuabudiwa PekeYake. Basi ni vipi mnaacha kumuabudu Yeye na mnaelekea kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa viumbe Vyake.
Mkimkanusha Mola wenu, enyi watu, mkaacha kumuamini na msiwafuate Mitume Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na nyinyi, Hana haja kwenu, na nyinyi ndio mnaomuhitajia, na Haridhiki na ukanushaji wa waja Wake, wala Hawaamrishi hilo. Hakika ni kwamba Analoridhika nalo kwao ni wazishukuru neema Zake juu yao. Na hakuna nafsi yoyote itakayobeba dhambi za nafsi nyingine. Kisha kurudi kwa Mola wenu ndio mwisho wenu, na hapo Awapashe habari ya matendo yenu na Awahesabu kwayo. Hakika Yeye ni Mjuzi sana wa siri za nafsi na yanayofichwa na vifua.
Na binadamu akipatwa na balaa, shida na maradhi humkumbuka Mola wake akataka nusura Yake na akamuomba, kisha Akimjibu na Akamuondolea shida yake na akampa neema Zake, huwa yuwasahau yale maombi yake aliyoyafanya kwa Mola wake alipomhitajia, na akawa atamshirikisha mwingine pamoja na Yeye, ili ampotoe mwingine amuepushe na kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtii. Mwambie, ewe Mtume, kwa kumuonya, «Starehe na ukafiri wako muda mchache mpaka kufa kwako na kumalizika kipindi chako cha kuishi, hakika wewe ni miongoni mwa watu wa Motoni wenye kukaa milele humo.»
Je, kafiri huyu anayejistarehesha na ukafiri wake ni bora au ni yule anayemuabudu Mola wake na kumnyenyekea, anatumia nyakati za usiku kusimama kwenye Ibada na kumsujudia, anaogopa adhabu ya Akhera na kutarajia rehema ya Mola wake? Sema, ewe Nabii, «Je, wanalingana wale wanaomjua Mola wao na dini yao ya haki na wale wasiojua chochote katika hayo?» Hawalingani. Kwa hakika wanaokumbuka na kujua tafauti ni wale wenye akili timamu.
Sema, ewe Nabii, kuwaambia waja wangu wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, «Mcheni Mwenyezi Mungu kwa kumtii na kujiepusha na matendo ya kumuasi.» Na wale waliofanya wema katika dunia hii kwa kumuabudu Mola wao na kumtii watapata wema huko Akhera, nao ni pepo, na wema huko duniani, ambao ni afya, riziki, ushindi na vinginevyo. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu, basi hamieni humo muende pale ambapo mtamuabudu Mola wenu na mtamakinika kusimamisha Dini yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Atawapa wenye kuvumilia malipo yao mema huko Akhera bila mpaka wala hesabu wala kipimo. Huku ni kuyafanya makubwa malipo ya wenye kusubiri na thawabu zao.
Sema, ewe Mtume, uwaambie watu, «Mwenyezi Mungu Ameniamrisha mimi na anayenifuata kumtakasia Yeye ibada, Peke Yake, bila mwingine,
na Ameniamrisha niwe wa kwanza kujisalimisha miongoni mwa ummah wangu, akasalimu amri Kwake kwa kumpwekesha na kumtakasia Ibada na akajiepusha na kila kisichokuwa Yeye miongoni mwa waungu.
Sema, ewe Mtume, uwaambie watu, «Mimi ninachelea nikimuasi Mola wangu, katika kile alichoniamuru cha kumuabudu na kumtakasia katika kumtii, adhabu ya Siku hiyo ambayo kituko chake ni kikubwa.
Sema, ewe Mtume, «Kwa hakika Mimi ninamuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, nikimtakasia ibada yangu na utiifu wangu.
Basi nyinyi, enyi washirikina, abuduni mnachotaka badala ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa mizimu na masanamu na visiokuwa hivyo katika viumbe Vyake, kwani hilo halinidhuru mimi chochote.» Na hili ni onyo na tahadharisho kwa anayemuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na akamshirikisha mwingine pamoja na Yeye. Sema, ewe Mtume, «Hakika wale wenye hasara kikweli ni wale watakaohasirika nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama.» Na hiyo ni kwa sababu ya kuwapoteza duniani na kuwapotosha na njia ya Imani. Jua utanabahi kwamba hawa washirikina kupata hasara ya nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama ndiko kupata hasara kuliofunuka waziwazi.
Hao wenye kupata hasara watawekewa juu yau Siku ya Kiyama, wakiwa ndani ya Jahanamu, vipande vya adhabu juu yao vinavyotokana na Moto, kama kwamba ni sakafu zilizojengewa na pia chini yao. Adhabu hiyo yenye sifa hizo ndio ile ambayo Mweyezi Mungu anawaogopesha nayo waja Wake ili wajihadhari nayo. Hivyo basi, enyi waja wangu, nicheni kwa kuzifuata amri zangu na kujiepusha na matendo ya kuniasi.
Na wale waliojiepusha kumtii Shetani na kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na wakatubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuabudu na kumtakasia Dini, basi hao wana bishara njema duniani ya kutajwa vyema na kuafikiwa na Mwenyezi Mungu, na bishara njema huko Akhera ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na starehe za daima Peponi. Basi wape habari njema, ewe Nabii, waja wangu
ambao wanasikiliza maneno na kufuata yaliyo sawa zaidi. Na maneno mazuri zaidi na yaliyo sawa zaidi ni maneno ya Mwenyezi Mungu kisha ni maneno ya Mtume Wake. Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaafikia kwenye usawa na haki na akawaongoza kwenye tabia na matendo bora zaidi; hao ndio watu wenye akili zilizotimia.
Je, yule ambaye lilipasa juu yake neno la adhabu, kwa kuendelea kwenye upotevu na upotovu wake, kwani huna, ewe Mtume, njia yoyote ya kumuongoa. Je, unaweza kumuokoa aliye Motoni? Wewe si mwenye kuweza hilo.
Lakini wale waliomcha Mola wao, kwa kumtii na kwa kumtakasia ibada, watakuwa na vyumba, huko Peponi, vilivyojengewa baadhi yake juu ya vingine, ambavyo chini ya miti yake mito inapita. Mwenyezi Mungu amewaahidi (vyumba hivyo) waja Wake wachamungu, ahadi ambayo ni yenye kutimia kwa uhakika, na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi,
Je, huoni, ewe Mtume, kuwa Mwenyezi Mungu Anateremsha mvua kutoka mawinguni, akaitia ardhini, akaifanya ni mikondo yenye kuchimbuka na maji yenye kutiririka, kisha anatoa kwa maji hayo mimea yenye rangi tafauti na aina mbalimbali, kisha inakauka baada ya ubichi wake na mng’aro wake, hapo utaiona imebadilika kuwa rangi ya manjano, kisha Anaifanya kuwa ni mapepe yaliyovunjikavunjika na kumumunyuka? Kwa hakika, katika kitendo hiko cha Mwenyezi Mungu pana ukumbusho na mawaidha kwa wenye akili timamu.
Je, yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemkunjua kifua chake, akabahatika kuukubali Uislamu, kuufuata na kuuamini, akawa yuko kwenye uwazi wa jambo lake na uongofu kutoka kwa Mola wake, je ni kama yule ambaye hayuko hivyo? Hao wawili hawalingani. Basi ole wao na maangamivu wale ambao nyoyo zao zilikuwa ngumu na zikajiepusha na utajo wa Mwenyezi Mungu. Hao wako kwenye upotevu ulio kando na haki waziwazi.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Aliteremsha Mazungumzo mazuri zaidi kuliko yote, nayo ni Qur’ani tukufu, inayofanana katika uzuri wake, upangikaji wake na kutotafautiana kwake, ndani yake mna hadithi, hukumu, hoja na dalili zilizo wazi. Kusomwa kwake kunarudiwa na ule wingi wa kuikariri hauifanyi ichokeshe. Isomwapo huifanya miili ya wenye kuisikia itetemeke na zitikisike ngozi za wale wanaomuogopa Mola wao, kwa kuathirika na yale yaliyomo ndani yake ya kutisha na kuonya, kisha zikalainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kufurahia bishara iliyomo ya ahadi njema na mahimizo ya kufanya kheri. Kuathirika huko na Qur’ani ni uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Anayempoteza asiiamini hii Qur’ani kwa sababu ya ukafiri wake na ushindani wake, basi hana muongozi mwenye kumuongoa na kumuafikia.
Je, Yule atakayetupwa Motoni akiwa amefungwa, akawa hawezi kujikinga na Moto isipokuwa kwa uso wake, kwa ukafiri wake na upotevu wake, ni bora au ni yule anayestarehe Peponi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amemuongoa? Na madhalimu Siku hiyo wataambiwa, «Onjeni madhara ya yale mliokuwa mkiyachuma duniani ya kumuasi Mwenyezi Mungu.
Wale waliokuwa kabla ya watu wako, ewe Mtume, waliwakanusha Mitume wao, hivyo basi adhabu ikawajia kwa namna ambayo hawakuhisi kuja kwake.
Basi Mwenyezi Mungu Akawaonjesha ummah waliokanusha adhabu na unyonge duniani, na Akawaandalia adhabu kali zaidi na ngumu zaidi huko Akhera. Lau hawa washirikina wangalijua, kuwa kile kilichowashukia ni kwa sababu ya ukafiri wao na ukanushaji wao, wangaliwaidhika.
Na kwa hakika tumewapigia hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu kila mfano katika mifano ya watu wa kame zilizopita, kwa kuwatisha na kuwaonya, ili wakumbuke na wakomeke na lile ambalo wako nalo la kumkufuru Mwenyezi Mungu.
Na tumeijaalia hii Qur’ani ni kwa lugha ya Kiarabu, yenye matamshi yaliyofunuka wazi na yenye maana mepesi yasiyo na uchanganyifu wala upotofu, huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo yake.
Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa mtumwa aliyemilikiwa na washirika wenye kuteta, na mtumwa mwingine aliyekuwa ni wa mmiliki mmoja tu, akawa yuwajua matakwa yake na yanayomridhisha. Je, mfano wa wawili hao unalingana? Basi Hivyo ndivo alivyo mshirikina. Yeye yuko katika hali ya mshangao na shaka, na Muumini yuko katika raha na utulivu. Sifa njema kamilifu zilizotimia ni za Mwenyezi Mungu, Peke Yake, lakini washirikina hawaijui haki wakaifuata.
Wewe ni mwenye kufa, ewe Mtume, na wao ni wenye kufa,
kisha nyote, Siku ya Kiyama. Kwa Mola wenu mtagombana, hapo Ahukumu baina yenu kwa uadilifu na usawa.
Hakuna yoyote dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo, kwa kumnasibishia sifa isiyofaa kusifika nayo, kama vile kuwa na mshirika na mtoto, au akasema, «Mimi nimeletewa wahyi,» na hali yeye hakuletewa wahyi wa kitu chochote. Na hakuna dhalimu zaidi kuliko yule aliyeikanusha haki iliyoteremka kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kwani si yako huko Motoni mashukio na makazi kwa waliomkufuru Mwenyezi Mungu na wasimuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie? Ndio, yako.
Na yule aliyekuja na ukweli wa maneno na vitendo, miongoni mwa Manabii na wafuasi wao, na akaukubali kiimani na kivitendo, hao ndio waliokusanya sifa za uchamungu, akiwa mbele yao yule aliye mwisho wa Manabii na Mitume, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale wenye kumuamini, wanaoifuata Sheria yake kivitendo miongoni mwa Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, kisha wale wenye kuja baada yao mpaka Siku ya Malipo.
Wao watayapata wanayoyataka kwa Mola wao miongoni mwa aina ya vitu vya ladha na matamanio. Hayo ndiyo malipo ya anayemtii Mola wake vile inavyopasa kutiiwa na akamuabudu vile inavyopasa kuabudiwa.
Ili Mwenyezi Mungu Awafutie yale maovu zaidi ya matendo waliyoyafanya ulimwenguni kwa sababu ya kile walichokifanya cha kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kutubia makosa waliyoyatenda huko, na ili Mwenyezi Mungu Awalipe mema, kwa utiifu wao ulimwenguni, malipo mazuri zaidi ya matendo ambayo walikuwa wakiyafanya, nayo ni Pepo,
Je, kwani Mwenyezi Mungu si Mwenye kumtosheleza mja Wake Muhammad vile vitisho vya washirikina na vitimbi vyao kuwa wao hawatamfikia kwa ubaya wowote? Ndio, Yeye Atamtosheleza katika jambo la Dini yake na dunia yake, na Atamtetea dhidi ya yoyote anayemtaka kwa ubaya. Na wao wanakutisha, ewe Mtume, na waungu wao wanaodai kuwa watakudhuru. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameondoa msaada Wake kwake na Akamfanya apotee njia ya haki, basi huyo hana muongozi wa kumuongoza Kwake.
Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuafikia kumuamini Yeye na kufanya matendo yanayoambatana na Kitabu Chake na kumfuata Mtume Wake, basi huyo hana mwenye kumpoteza na kumpotosha na haki ambayo amesimama nayo. Kwani Mwenyezi Mungu si Mshindi katika kuwatesa viumbe Wake waliomkufuru na wale waliomuasi?
Na unapowauliza, ewe Mtume, hawa washirikina wanaomuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, «Ni nani aliyeziumba hizi mbingu na ardhi?» watasema, «Aliyeziumba ni Mwenyezi Mungu.» Kwa hivyo wao wanamkubali Muumba. Basi waambie, «Je, waungu hawa mnaowashirikisha na Mwenyezi Mungu wanaweza kuniepushia makero ambayo Mwenyezi Mungu Amenikadiria au kuniondolea mambo ninayoyachukia yaliyonifika? Na je, wanaweza wao kuzuia manufaa aliyonisahilishia Mwenyezi Mungu nisiyapate au kunizuilia rehema ya Mwenyezi Mungu isinifikie?» Wao watasema, «Hawawezi hilo.» Waambie, «Mwenye kunitosheleza na kuniridhisha mimi ni Mwenyezi Mungu. Kwake yeye wanategemea wenye kutegemea katika kuleta yanayowafaa na kuzuia yanayowadhuru. Yule ambaye kwenye mkono wake peke yake kuna toshelezo, Yeye Ndiye Mwenye kunitosha na Atanikifia kila linalonitia hamu.
Sema, ewe Mtume, uwaambie watu wako wenye ukaidi, «Fanyeni matendo kwa namna inayoridhisha nafsi zenu, kwa kuwa mmemuabudu asiyestahiki kuabudiwa na asiye na amri ya jambo lolote. Mimi ni mwenye kufanya yale niliyoamrishwa ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake katika maneno yangu na vitendo vyangu.
Na mtajua ni yupi atakayejiwa na adhabu yenye kumfanya mnyonge katika maisha ya ulimwenguni na atakayeshukiwa na adhabu ya daima kesho Akhera, haitamuepuka wala haitamuondokea.
Hakika sisi tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa haki ikiwa ni yenye kuwaongoza viumbe wote kwenye njia ya uongofu. Basi mwenye kuongoka kwa mwangaza wake na akayatumia yaliyomo ndani yake na akasimama imara kufuata njia yake, basi manufaa ya kufanya hilo yatamrudia mwenyewe. Na mwenye kupotea baada ya kubainikiwa na uongofu, basi madhara yake yatamrudia mwenyewe, na hilo halitamdhuru Mwenyezi Mungu kitu chochote. Na hukuwa wewe, ewe Mtume, ni mwakilishwa wa kuyatunza matendo yao, kuwahesabu kwa hayo na kuwalazimisha unayoyataka, jukumu lako wewe si lingine isipokuwa ni kufikisha ujumbe.
Mwenyezi Mungu Ndiye Anayezikamata nafsi wakati zinapokufa. Kufa huku ni kufa kukubwa, kufa kwa kushukiwa na mauti kwa ajali kukoma. Na zile nafsi ambazo hazikufa Anazikamata katika hali ya kulala kwake, nako ndiko kufa kudogo. Hivyo basi Akazizuia, kati ya hizi nafsi mbili, ile Aliyoitolea uamuzi ife , nayo ni ya yule aliyekufa, na anaiachilia nafsi nyingine mpaka ikamilishe muda wake wa kuishi na riziki yake, nako ni kuirudisha kwenye mwili wa mwenye nafsi hiyo. Kwa kweli, katika kule kukamata kwa Mwenyezi Mungu nafsi ya aliyekufa na aliyelala na kuiachilia nafsi ya aliyelala na kuizuia nafsi ya aliyekufa kuna dalili waziwazi za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa anayefikiria na kuzingatia.
Au kwani hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu wamewachukua badala Yake Yeye waungu wao wanaowaabudu wakawafanya ni waombezi wakuwaombea kwa Mwenyezi Mungu katika haja zao? Waambie, «Je mnawafanya ni waombezi kama mnavyodai, ingawa waungu hao hawamiliki chochote na hawafahamu kamwe kuwa nyinyi mnawaabudu?
Waambie, ewe Mtume, hao washirikina, «Ni wa Mwenyezi Mungu uombezi wote. Ni Yake Yeye mamalaka ya mbinguni na ardhini na vilivyoko baina yake. Amri yote ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na hakuna yoyote atakayeombea mbele Yake isipokuwa kwa idhini Yake. Yeye Ndiye Anayemiliki mbingu na ardhi na anayeendesha mambo yake. Lilo wajibu ni kutakwa uombezi kutoka kwa anayeumiliki na atakasiwe Yeye kwa ibada, na usitakwe kutoka kwa waungu wasiodhuru wala kunufaisha, kisha Kwake Yeye mtarudishwa baada ya kufa kwenu ili mhesabiwe na mlipwe.
Na Anapotajwa Mwenyezi Mungu Peke Yake zinachukia nyoyo za wasioamini Marejeo na Ufufuzi baada ya kufa, na wanapotajwa wale wasiokuwa Yeye miongoni masanamu, mizimu na wategemewa huwa wakifurahika kwa kuwa ushirikina unaafikiana na matamanio yao.
Sema, «Ewe Mwenyezi Mungu! Ewe Muumba mbingu na ardhi, Mwenye kuanzisha kuzitengeneza bila kuwa na mfano uliotangulia! Mjuzi wa siri na dhahiri! Wewe unatoa uamuzi baina ya waja wako Siku ya Kiyama katika yale ambayo walikuwa wakitafautiana juu yake ya maneno kuhusu wewe, ukubwa wako, utawala wako na kuhusu kukuamini wewe na kumuamini Mtume wako. Niongoze mimi kwenye haki ambayo kumetafautiana juu yake kwa amri yako. Hakika wewe unamuongoza unayemtaka kwenye njia iliyolingana sawa.» Hii ilikuwa ni miongoni mwa dua za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, nayo ina mafundisho kwa waja watake himaya kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na wamuombe kwa mjina Yake mazuri na sifa Zake tukufu.
Na lau hao wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu wangalikuwa nacho kila kilichoko kwenye ardhi miongoni mwa mali, vitu vya thamani na vingine mfano wake pamoja navyo kuongezea, wangalikitoa Siku ya Kiyama ili wajikomboe kwacho na adhabu mbaya. Na lau wangalikitoa na wakataka kujikomboa kwacho hakingalikubaliwa kutoka kwao na hakingaliwafalia kitu chochote kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na itawadhihirikia wao Siku hiyo amri ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake wasizokuwa wakizidhania duniani kuwa zitawashukia.
Na yatawadhihirikia hao wakanushaji, Siku ya kuhesabiwa, malipo ya maovu yao waliyoyatenda, kwa kuwa walimnasibishia Mwenyezi Mungu sifa isiyolingana na Yeye, na wakafanya maasia katika maisha yao, na itawazunguka adhabu kali kila upande ikiwa ni mateso kwao kwa kulifanyia shere onyo la adhabu ambayo Mtume alikuwa akiwaahidi kuwa itawapata wakawa hawaitii maanani.
Na ikimpata mwanadamu shida na madhara humuomba Mola wake amuondolee, na tunapomuondolea yaliyompata na tukampa neema kutoka kwetu hurudi kumkanusha Mola wake na kukataa wema Wake na huwa akisema, «Haya niliyopewa yatokamana na ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuwa mimi ninafaa na ninastahiki kuyapata. Bali huo ni mtihani wa Mwenyezi Mungu kuwatahini waja Wake, ili Atazame ni yupi anayemshukuru kwa kumtenga na anayemkanusha. Lakini wengi wao, kwa ujinga wao na dhana zao mbaya, hawajui kuwa hayo ni mavuto kideogo-kidogo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni mtihani kwao kuhusu kushukuru neema.
Kauli kama hii ilisemwa na ummah waliopita wenye kukanusha, na yasiwafalie kitu, ilipowajia adhabu, yale mali ambayo walikuwa wakiyachuma na watoto.
Yakawapata wale waliyosema kauli hii, miongoni mwa ummah waliopita, mateso ya matendo mabaya waliyoyachuma, hivyo basi wakaharakishiwa laana katika maisha ya duniani. Na wale waliojidhulumu nafsi zao katika watu wako, ewe Mtume, na wakasema kauli hii, yatawapata mateso ya yale mabaya waliyoyachuma kama yaliyowapata waliokuwa kabla yao, na hawakuwa wao ni wenye kumponyoka Mwenyezi Mungu wala kumshinda.
Kwani hao hawajui kwamba riziki ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu haimaanishi kuwa aliyeruzukiwa ana hali njema na kwamba Mwenyezi Mungu Ana hekima nyingi, Anamkunjulia riziki Anayemtaka katika waja Wake, awe mwema au muovu, na Anambania Anayemtaka katika wao? Hakika katika kukunjua na kubana riziki kuna dalili zilizo wazi kwa watu wanaoamini amri ya Mwenyezi Mungu na kuifanyia kazi.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia waja wangu waliojidhulumu nafsi zao kwa kuyajia madhambi ambayo nafsi zao zinawaitia, «Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa wingi wa madhambi yenu, kwani Mwenyezi mungu Anasamehe dhambi zote kwa mwenye kutubia kutokana nayo na akayaacha namna yatakavyokuwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya wenye kutubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu.
«Na rudini kwa Mola wenu, enyi watu, kwa kutii na kutubia, na mnyenyekeeni kabla hayajawashukia mateso Yake, kisha hakuna yoyote Atakayewanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
«Na fuateni bora zaidi wa kile kilichoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, nacho ni Qur’ani tukufu, na yote ni njema, basi jilazimisheni kufuata amri zake na jiepusheni na makatazo yake kabla haijawajia nyinyi adhabu kwa ghafla na nyinyi hamuijui.»
«Na mtiini Mola wenu na tubieni Kwake ili isije nafsi ikajuta na ikasema, ‘Ee hasara yangu kwa matendo mema niliyoyapoteza ulimwenguni katika yale Aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na nikafanya kasoro katika kumtii na kutekeleza haki Yake,! Na ingawa ulimwenguni nilikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wakiifanyia shere amri ya Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, Mtume Wake na waliomuamini.’
«Au ikasema, ‘Lau Mwenyezi Mungu Angaliniongoza kwenye Dini Yake ningalikuwa ni miongoni mwa wenye kujikinga na ushirikina na maasia.’»
«Au ikasema, itakapo kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu imeizunguka Siku ya Kiyama, ‘Natamani nipatiwe nafasi ya kurudi kwenye maisha ya kilimwengu nikawa huko ni miongoni mwa wenye kufanya wema kwa kumtii Mola wao na kufanya matendo yaliyoamrishwa na Mitume.’»
Maneno siyo kama unavyosema, Kwa hakika aya zangu zilizo wazi zenye kuitolea ushahidi haki zilikujia ukazikanusha, ukazifanyia kiburi usizikubali na usizifuate na ukawa ni miongoni mwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.
Na Siku ya Kiyama utawaona hao wakanushaji, waliomsifu Mola wao kwa sifa zisizolingana na Yeye na wakamnasibisha Yeye na mshirika na mwana, nyuso zao zimekuwa nyeusi. Si ndani ya Jahanamu kuna mashukio na makao kwa aliyemfanyia Mwenyezi Mungu kiburi akakataa kumpwekesha na kumtii? Ndio.
Na Mwenyezi Mungu Atawaokoa na Moto wa Jahanamu na adhabu yake wale waliomcha Mola wao kwa kutekeleza faradhi Alizoziamrisha na kujiepusha na yale Aliyoyakataza kwa kufuzu kwao na kutimia matakwa yao, nako ni kufaulu kupata Pepo. Hawataguswa na kitu chochote cha adhabu wala hawatazisikitikia hadhi za duniani walizozikosa.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Muumba wa vitu vyote, Ndiye Mola wa hivyo vitu na Ndiye Mwenye kuviendesha. Na Yeye ni Mtunzi wa kila kitu. Anayaendesha mambo yote ya viumbe Vyake.
Ni za Mwenyezi Mungu funguo za hazina za mbinguni na ardhini, Anatoa kutoka kwenye hazina hizo kuwapa viumbe Vyake namna Anavyotaka. Na wale waliozikanusha aya za Qur’ani na dalili wazi zilizomo, hao ndio wenye kupata hasara ulimwenguni kwa kutoafikiwa kuamini, na kesho Akhera kwa kukaa milele Motoni.
Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina wa watu wako, «Je, yule asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi wajinga, mnanishauri nimuabudu na hali ibada haifai kufanyiwa kitu chochote isipokuwa Yeye?»
Kwa hakika uliletewa wahyi wewe, ewe Mtume, na Mitume waliokuwa kabla yako kwamba lau ulimshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye amali zako zingalibatilika na ungalikuwa ni miongoni mwa walioangamia waliopata hasara, hivyo basi ukapata hasara ya dini yako na Akhera Yako, kwani pamoja na ushirikina haikubaliwi amali njema.
Bali Mwenyezi Mungu muabudu, ewe Mtume, kwa kumtakasia ibada Peke Yake Asiye na mshirika, na uwe ni miongoni mwa wenye kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu.
Na hawa washirikina hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu vile Anavyostahiki kuadhimishwa, kwa kuwa wamemuabudu asiyekuwa Yeye pamoja na Yeye miongoni mwa wale wasionufaisha wala kudhuru, wakamfanya muumbwa, pamoja na uelemevu wake, kuwa ni sawa na Muumba Mtukufu, Ambaye kotokana na uweza Wake mkubwa ni kwamba ardhi yote itakuwa iko mkononi Mwake Siku ya Kiyama, na mbingu zitakuwa zimekunjwa kwa mkono Wake wa kulia. Ametakasika Mwenyezi Mungu na kutukuka kwa kuepukana na kile wanaomshirikisha nacho hao washirikina. Katika aya hii pana dalili ya kuthibitisha kushika kwa mkono, mkono wa kulia na kukunja kwa Mwenyezi Mungu kama vile inavyolingana na haiba Yake na utukufu Wake bila kueleza Yuko vipi wala kufananisha.
Na kutapulizwa kwenye baragumu na hapo atakufa kila aliye kwenye mbingu na ardhi, isipokuwa anayemtaka Mwenyezi Mungu asife. Kisha Malaika Atapuliza mara ya pili kwenye baragumu akitangaza kufufuliwa viumbe wapate kuhesabiwa mbele ya Mola wao, na wakitahamaki wao wamesimama kutoka makaburini mwao wanangojea yale Atakayowafanyia Mwenyezi Mungu.
Na ardhi itatoa mwangaza Siku ya Kiyama, Atakapo kujitokeza Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ili kutoa hukumu, na hapo Malaika wautandaze ukurasa wa kila mtu, na Mitume waletwe na mashahidi wa kila ummah, ili Mwenyezi Mungu Awaulize manabii kuhusu ufikishaji ujumbe kwa ummah wao na majibu waliopata kutoka kwao. Kadhalika waje ummah wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu, ili kuutolea ushahidi ufikishaji wa Mitume waliotangulia kwa ummah wao iwapo watakataa kuwa walifikishiwa. Na hapo ushahidi uthibiti juu ya ummah wote, na Mwenyezi Mungu Atoe hukumu baina ya waja kwa uadilifu uliotimia. Na wao hawatadhulumiwa kitu chochote kwa kupunguziwa thawabu au kwa kuongezewa mateso.
Na hapo Mwenyezi Mungu Aipe kila nafsi malipo ya matendo yake, mazuri na mabaya. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutuka ni Kwake, Ndiye Anayejua zaidi yale waliyoyafanya duniani ya utiifu au ya uasi.
Na waongozwe wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kuelekezwa upande wa Jahanamu makundi kwa makundi, na watakapoifikia itafunguliwa milango yake saba na wale washika hazina wake waliowakilishwa kuisimamia hiyo Jahanamu. Na hao washika hazina watawakaripia kwa kusema, «Vipi nyinyi mlimuasi Mwenyezi Mungu na mkakataa kuwa Yeye ni Mola wa haki Peke Yake.? Kwani hamkutumiwa Mitume miongoni mwenu wanaowasomea aya za Mola wenu na kuwaonya na vituko vya Siku ya Leo?» Watasema wakikubali makosa yao, «Ndio, walitujia na ukweli Mitume wa Mola wetu na wakatuonya na Siku ya Leo, lakini lishathibiti neno la Mwenyezi Mungu kwamba adhabu Yake itawafikia wenye kumkanusha Yeye.»
Na wataambiwa wale wenye kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, kwa kuwatweza na kuwadhalilisha, «Ingieni kwenye milango ya Jahanamu, hali ya kukaa humo milele.» Ni mbaya mno mwisho wa wale wanaolifanyia kiburi jambo la kumuamini Mwenyezi Mungu na kufuata kivitendo sheria Yake.
Na wataongozwa wale waliomcha Mola wao, kwa kumpwekwsha na kufanya vitendo vya utiifu Kwake, wapelekwe Peponi, makundi kwa makundi. Na watakapoifikia na waombewe kuingia, milango yake itafunguliwa, na Malaika waliowakilishwa kuisimamia Pepo watawakongowea na watawaamkia kwa ucheshi na furaha kwa kuwa wamesafishika na athari za maasia na watawaambia, «Amani iwe juu yenu! Mmesalimika na kila baya. Hali zenu ni nzuri. Basi ingieni Peponi mkae milele humo.»
Na hapo Waumini watasema, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuhakikishia ukweli wa ahadi Yake Aliyotuahidi kupitia kwa ndimi za Mitume Wake, na Akaturithisha ardhi ya Pepo tukawa tunashukia kwenye ardhi hiyo popote pale tunapotaka. Ni mazuri yaliyoje malipo ya watu wema waliojitahidi kumtii Mola wao.»
Na utawaona Malaika, ewe Nabii, wameizunguka 'Arshi ya Mwingi wa rehema, wanamtakasa Mola wao na kumuepusha na kila kisichofaa kunasibishwa nacho, (na utaona kuwa) Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka Amehukumu baina ya viumbe kwa uhaki na uadilifu, Akawakalisha wenye kuamini Peponi na wenye kukufuru Motoni. Na hapo kutasemwa, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote kwa uamuzi Aliyoutoa baina ya watu wa Peponi na Motoni, shukrani ya kutambua wema na hisani na shukrani ya kutambua uadilifu na hekima.»
Icon