ترجمة سورة الإنشقاق

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الإنشقاق باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Pindi mbingu itakapopasuka na kudhihiri mawingu katika pasuko zake Siku ya Kiyama.
Na ikatii amri ya Mola wake ya kuwa ipasuke, na inastahili kufuata amri hiyo.
Na pindi ardhi itakapotandikwa na kukunjuliwa.
Na milima yake kuvunjwa-vunjwa Siku hiyo.
Na ikatii amri ya Mola wake ya kuwa ifanye hivyo, na inastahili kufuata amri hiyo.
Ewe binadamu, wewe unaenda kwa Mwenyezi Mungu na unafanya amali nzuri na mbaya, kisha utakutana na Yeye Siku ya Kiyama. Na huna budi kupata kutoka Kwake malipo mazuri zaidi ya amali yako njema au yanayolingana na amali yako mbaya.
Yule mwenye kupewa waraka wa amali zake kwa mkono wake wa kulia,
naye ni yule aliyemuamini Mola wake, atahesabiwa hesabu pesi.
Na atarudi kwa watu wake Peponi akiwa ni mwenye furaha.
Na yule mwenye kupewa waraka wa amali zake kwa nyuma ya mgongo wake,
naye ni yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu, ataita maangamvu na hasara,
na ataingia Motoni.
Hakika yeye alikuwa kwa watu wake ulimwenguni ni mwenye furaha na majivuno, hafikirii mwisho wake utakuwa namna gani.
Alidhani hatarudi kwa Muumba wake, akiwa hai, kwa kuhesabiwa.
Sivyo hivyo! Mwenyezi Mungu Atamrudisha kama alivomuumba na kumlipa kwa amali zake. Kwani Yeye kwake ni Mtambuzi na kwa hali yake ni Mjuzi kuanzia Alipomuumba mpaka kumfufua.
Mwenyezi Mungu Ameapa kwa wekundu wa pambizo za mbingu wakati wa kutwa jua.
Na kwa usiku na viunbe tofauti - tofauti vya kutambaa, kuruka na kutembea kwa miguu, uliokusanya.
Na kwa mwezi ukamilikapo mwangaza wake.
Mtapitia, enyi watu, miongo mbalimbali na hali tofauti :kutoka kwenye tone la manii, kuptia pande la damu, nofu la nyama hadi kutiwa roho, mpaka kufa na mpaka kufufuliwa. Haifai kwa kiumbe kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, afanyapo hilo atakuwa ameingia kwenye ushirikina.
Ni kitu gani kinachowazuia kumwamini baada ya aya zake kufafanuliwa kwao?
Na wana nini wao wanaposomewa Qur’ani hawamsujudii Mwenyezi Mungu wala hawajisalimishi kufuata yaliyokuja ndani yake?
Hakika tabia ya waliokufuru ni kuikanusha na kuikataa haki.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa ukaidi wao wanaouficha kwenye nyoyo zao hali wao wanajua kuwa yale yaliyoletwa na Qur’ani ni kweli.
Basi wape bishara, ewe Mtume, kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Amewaandalia adhabu yenye uchungu.
Lakini wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakatekeleza amri waliyofaradhiwa na Mwenyezi Mungu watakuwa na malipo, Siku ya Akhera, yasiyokatika wala kupungua.
Icon