ﰡ
Sifa njema zote asifiwe Mwenyezi Mungu kwa sifa Zake ambazo zote ni za ukamilifu, na kwa neema Zake za nje na za ndani, za Akhera na duniani. Muumba mbingu na ardhi na Muanzilishi wa hizo. Mwenye kuwafanya Malaika ni wajumbe kwa waja kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake, na kwa amri Yake anayoitaka na makatazo Yake. Na miongoni mwa ukubwa wa uweza wa Mwenyezi Mungu ni kuwafanya Malaika ni wenye mbawa, mbilimibili, tatutatu na nnenne, za kurukia: ili kukifikisha Alichoamrisha Mwenyezi Mungu. Katika uumbaji Wake Anaongeza Anachotaka. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Mjuzi, hakuna kitu kinachomshinda.
Chochote kile Anachowafungulia watu Mwenyezi Mungu miongoni mwa riziki, mvua, afya, ujuzi na neema nyinginezo, hakuna yoyote wa kuzuia rehema hii, na chochote kile anachokizuia hakuna yoyote baada Yake, Kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, anayeweza kukiachilia. Na Yeye Ndie Mshindi Mwenye kukitendesha nguvu kila kitu, Mwingi wa hekima Ambaye Anaiachilia rehema na Anaizuia kulingana na hekima Yake.
Enyi watu! Kumbukeni, kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu, neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Hakuna muumba wenu isipokuwa Mwenyezi Mungu, Anayewaruzuku nyinyi kwa mvua kutoka mbinguni, na kwa maji, madini na vinginevyo kutoka ardhini. Hapana Mola isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiye na mshirika. Basi vipi nyinyi mtaepushwa na kumpwekesha?
Na watu wako wakikukanusha, ewe Mtume, kwa hakika wamekanushwa Mitume kabla yako wewe. Na kwa Mwenyezi Mungu mambo yanaishia huko Akhera, basi hapo Atamlipa kila mmoja anachostahili. Katika hii pana kumliwaza Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Enyi watu! Hakika agizo la Mwenyezi Mungu la Ufufuzi, malipo mema na mateso ni kweli iliyothibiti, basi yasiwadanganye maisha ya duniani kwa matamanio yake na matakwa yake, wala asiwadanganye Shetani kuhusu Mwenyezi Mungu.
Hakika Shetani ni adui ya binadamu, basi mchukulieni ni adui na msimtii, hakika ni kwamba yeye anawaita wafuasi wake kwenye upotevu ili wawe ni katika watu wa Moto unaowaka.
Wale waliokataa kwamba Mwenyezi Mungu, Yeye Peke Yake, Ndiye Mola wa kweli, na wakakataa kile walichokuja nacho Mitume Wake, watakuwa na adhabu kali huko Akhera. Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, watapata msamaha kutoka kwa Mola wao na kufutiwa dhambi zao baada ya kuzifanya zisitirike, na watakuwa na malipo mema makubwa, nayo ni Pepo.
Je, yule ambaye Shetani anampambia matendo yake maovu ya kumuasi Mwenyezi Mungu, kukufuru na kuwaabudu wasiyekuwa Yeye miongoni mwa waungu na masanamu, akayaona ni mazuri yenye kupendeza, (Je, yeye) ni kama yule ambaye Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amemuongoza akaliona zuri kuwa ni zuri na ovu kuwa ni ovu? Hakika Mwenyezi Mungu Anampoteza Anayemtaka na Anamuongoza Anayemtaka. Basi usijiangamize kwa kuwa na huzuni juu ya ukanushaji wa hawa waliopotea. Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua maovu yao na Atawalipa kwa hayo malipo mabaya kabisa.
Na Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye Anapeleka upepo, ukatikisa mawingu, tukayaongoza hadi pale kwenye ardhi kavu, hapo mvua ikateremka, tukahuisha kwa mvua hiyo ardhi baada ya ukavu wake, na hapo mimea ikawa rangi ya kijani. Mfano wa kuhuisha huko, Mwenyezi Mungu Atawahuisha wafu Siku ya Kiyama.
Yoyote yule atakaye enzi ya duniani au Akhera, basi aitake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hilo halipatikani isipokuwa kwa kumtii Yeye, kwani enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kujienzi na kiumbe, Mwenyezi Mungu Atamdhalilisha; na Mwenye kujienzi na Muumba, Mwenyezi Mungu Atamtukuza. Kwake Yeye utajo wake utapanda, na tendo lema Analiinua juu. Na wale wenye kutenda mabaya watapewa adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaangamia na vitaharibika na havitawafaidisha kitu chochote.
Na Mwenyezi Mungu Alimuumba baba yenu Ādam kwa mchanga kisha Akajaalia kizazi chake kitokamane na maji matwevu, kisha Akawafanya nyinyi ni wanaume na wanawake. Na hakuna mwanamke yoyote anayeshika mimba wala anayezaa isipokuwa Analijua hilo. Na hakuna mtu anayepewa maisha marefu au umri wake ukapunguzwa isipokuwa hayo yamo ndani ya Kitabu kilichoko Kwake, nacho ni Ubao Uliohifadhiwa, kabla mamake hajashika mimba yake na kabla hajamzaa. Hayo yote Mwenyezi Mungu Ameyadhibiti ameyajua kabla hajamuumba, hayataongezwa yale aliyoandikiwa wala hayatapunguzwa. Hakika kule kuwaumba nyinyi, kuzijua hali zenu na kuziandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa ni jambo rahisi na sahali kwa Mwenyezi Mungu.
Na hazilingani bahari mbili: hii ni tamu yenye upeo wa utamu, ni laini kupita kooni, inaondosha kiu, na hii (nyingine) ni ya chumvi yenye uchumvi mkali. Na kutokana na kila mojawapo ya bahari mbili mnakula samaki wazuri wenye ladha ya kupendeza, na mnatoa pambo, ambalo ni lulu na marjani, la nyinyi kulivaa. Na utaviona vyombo ndani ya bahari hizo vinapasua maji, ili mkiwa mnatafuta kheri Zake katika biashara na megineyo. Katika haya kuna dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu na upweke Wake, na huenda nyinyi mkamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizi ambazo Amewaneemesha nazo.
Na Mwenyezi Mungu Anazitia nyakati za usiku ndani mchana, hivyo basi mchana ukarefuka kwa kadiri ya usiku uliopungua; na Anazitia nyakati za mchana ndani ya usiku, hivyo basi usiku ukarefuka kwa kadiri ya mchana uliopungua. Na Amedhalilisha jua na mwezi vikawa vinatembea kwa wakati maaalumu. Huyo aliyefanya hili ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Ni Wake Yeye ufalme wote. Na wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawamiliki hata utandu mwembamba unaozunguka koko ya tende.
Mnapowaomba, enyi watu, waabudiwa hawa badala ya Mwenyezi Mungu, hawasikii maombi yenu, na lau wangalisikia, kwa kukisia, hawangaliwaitikia nyinyi. Na Siku ya Kiyama, watajiepusha na nyinyi. Na hakuna yoyote wa kukupasha habari, ewe Mtume, mkweli zaidi kuliko Mwenyezi Mungu, Aliye Mjuzi, Aliye Mtambuzi.
Enyi watu! Nyinyi ndio wahitaji wa Mwenyezi Mungu katika kila kitu, hamjitoshelezi Naye hata kiasi cha kupepesa jicho. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye kujitosheleza na watu na kila kitu miongoni mwa viumbe Vyake, Mwenye kushukuriwa kwa dhati Yake na majina Yake na sifa Zake, Anaeshukuriwa kwa neema Zake. Kwani kila neema waliyo nayo watu inatoka Kwake. Sifa njema zote ni Zake na shukrani kwa kila namna.
Akitaka Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi, enyi watu, na Awalete watu wengine Ambao watamtii na watamuabudu Peke Yake.
Na halikuwa hili la kuwaangamiza nyinyi na kuwaleta viumbe wasiokuwa nyinyi ni jambo lisiowezekana kwa Mwenyezi Mungu, bali hilo ni jambo jepesi na rahisi
Na kiumbe yoyote Aliyefanya dhambi hatabeba dhambi za mtu mwingine. Na mtu yoyote aliyelemewa na dhambi, akiomba mwenye kumbebea dhambi zake, hatapata mwenye kumbebea chochote, hata kama yule aliyemuomba ana ujamaa wa karibu na yeye, kama baba au ndugu na mfano wao. Hakika ni kwamba wewe, ewe Mtume, unawaonya wale wanaoogopa adhabu ya Mola wao pamoja na kuwa wao hawaioni na wakatekeleza Swala inavyotakikana itekelezwe. Na mwenye kujisafisha na ushirikina na maasia mengine, basi yeye anajisafisha nafsi yake. Na kwa Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ndio marejeo ya viumbe wote na mwisho wao, hapo Amlipe kila mmoja kile anachostahiki.
Na kipofu asiyeiona Dini ya Mwenyezi Mungu halingani na yule mwenye kuona ambaye anaiona njia ya haki na anaifuata.
Na giza la ukafiri halilingani na mwangaza wa Imani,
wala kivuli hakilingani na upepo wa joto.
Na wale waliohuika nyoyo kwa kukuamini hawalingani na wale waliokufa nyoyo kwa kukanusha. Hakika Mwenyezi Mungu Anamsikilizisha Anayemtaka asikie kwa kufahamu na kukubali. Na wewe, ewe Mtume, si mwenye kuwasikilizisha walio ndani ya makaburi. Na kama usivyoweza kuwasikilizisha wafu makaburini mwao, pia hutawasikilizisha hawa makafiri kwa kuwa nyoyo zao zimekufa.
Wewe hukuwa isipokuwa ni mwenye kuwaonya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na mateso Yake.
Sisi tumekutumiliza kwa haki, nayo ni kumuamini Mwenyezi Mungu na Sheria za Dini, hali ya kuwapa bishara ya Pepo wale wenye kukuamini na wakaufuata uongofu wako kivitendo, na hali ya kuwaonya Moto wale waliokukanusha na wakakuasi. Na hakuna taifa lolote la watu isipokuwa limejiwa na muonyaji wa kuwaonya mwisho mbaya wa ukafiri wao na upotevu wao.
Na wanapokukanusha washirikina hawa , basi wale waliopita kabla yao waliwakanusha Mitume wao ambao waliwajia na miujiza iliyo wazi yenye kutolea ushahidi unabii wao, na waliwajia na Vitabu, ambavyo ndani yake zimekusanywa hukumu nyingi, na (waliwajia na) Kitabu chenye kutoa mwangaza chenye kubainisha njia ya kheri na shari.
Kisha nikawakamata wale waliokanusha na kuwapa aina mbalimbali za adhabu. Basi angalia kulikuwa namna gani kukataa kwangu matendo yao na kule kuwashukia wao mateso yangu?
Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu Ameteremsha kutoka juu maji, tukainywesha kwayo miti iliyo ardhini, tukatoa kwenye miti hiyo matunda yenye rangi tofauti, miongoni mwazo ni nyekundu na miongoni mwazo nyeusi na manjano na zisizokuwa hizo? Na tumeumba majabalini njia zenye rangi tofauti, nyeupe na nyekundu. Na tumeumba miongoni mwa majabali, majabali meusi sana.
Na miongoni mwa watu na wanyama, ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo tumeumba wakiwa rangi tofauti vilevile. Kati ya hao kuna wekundu, weupe weusi na wenye rangi nyinginezo, kama vile kutofautiana rangi za matunda na majabali. Hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu na kujikinga na mateso Yake kwa kumtii na kujiepusha kumuasi ni wale wanaomjua Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake,sifa Zake na Sheria Zake, na uweza Wake juu ya kila kitu ambao miongoni mwavyo ni kutofautiana viumbe hivi pamoja na kuwa sababu yake ni moja, na wanayatia akilini yaliyomo ndani ya mawaidha na mazingatio. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye nguvu Asiyeshindwa, Mwingi wa kusamehe Anawapa malipo mema watiifu, na Anawasamehe.
Hakika ya wale wanaosoma Qur’ani na wakaifanyia kazi, wakaendelea daima kuswali kwa nyakati zake na wakatumia kile tulichowaruzuku miongoni mwa aina ya matumizi ya lazima na ya yanayopendekezwa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wana matumaini kwa hayo kufanya biashara isiyoenda na isiyoanguka, nayo ni kuridhiwa na Mola wao na kufaulu kupata malipo mema mengi Yake.
Ili Awatimizie Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, malipo mema ya matendo yao yakiwa kamili bila kupunguzwa, na wataongezewa mema kwa fadhila Zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehefu sana wa makosa yao, ni Mwingi wa shukrani kwa mema yao, Atawalipa kwa mema hayo malipo mazuri mengi.
Na Qur’ni tuliyokuteremshia wewe, ewe Mtume, ndiyo haki inayosadikisha Vitabu Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume Wake kabla yako. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mambo ya waja Wake, ni Mwenye kuviona vitendo vyao, na Atawalipa wema kwa hayo.
Kisha tukawapa Qur’ani, baada ya ummah waliopita kuangamia, wale tuliowachagua miongoni mwa umati wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie: kati yao kuna aliyeidhulumu nafsi yake kwa kufanya baadhi ya maasia, na kati yao kuna aliyekuwa wastani, naye ni yule mwenye kutekeleza yaliyo wajibu na kuepuka yaliyoharamishwa, na katika wao kuna mwenye kutangulia kufanya mambo ya kheri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, yaani mwenye kukimbilia na kujitahidi kufanya amali njema, za faradhi na za ziada. Na kupewa Kitabu huko na kuchaguliwa ummah huu ndio nyongeza kubwa.
Pepo za makazi ya daima kwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewarithisha Kitabu Chake, watapambwa huko kwa vikuku vya dhahabu na kwa lulu. Na mavazi yao ya kawaida huko Peponi ni hariri, yaani: nguo laini.
Na watasema watakapoingia Peponi, «Sifa njema zote na shukrani ni za Mwenyezi Mungu Ambaye ametuondolea kila jambo la huzuni. Hakika Mola wetu ni Mwingi wa msamaha, kwa kuwa Anatusamehe sisi madhambi madogo, ni Mwingi wa shukrani, kwa kuwa Ameyapokea mazuri yetu na Ameyaongeza.
Na Yeye Ndiye Aliyetushukisha Nyumba ya Pepo kwa fadhila Zake, haitatugusa humo usumbufu wala uchovu.
Na wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, watakuwa na Moto wa Jahanamu uliowashwa. Hakutatolewa uamuzi juu yao kuwa wafe wakapata kufa na kupumzika, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Mfano wa malipo hayo, Mwenyezi Mungu Anamlipa kila mwenye kuendelea kwenye ukafiri na kuwa na ukakamavu juu yake.
Na hawa makafiri watapiga kelele kwa ukali wa adhabu ndani ya Moto wa Jahanamu wakiomba kuokolewa, «Mola wetu! Tutoe kwenye Moto wa Jahanamu na uturudishe duniani tupate kufanya matendo mema ambayo siyo yale tuliokuwa tukiyafanya katika uhai wetu wa duniani, tupate kuamini badala ya kukanusha.» Hapo Mwenyezi Mungu Awaambie, «Kwani hatukuwapa katika kipindi cha uhai kadiri inayotosha ya umri kwa mwenye kutaka kuwaidhika awaidhike, na akawajia Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na pamoja na hivyo msiwaidhike? Basi onjeni adhabu ya Jahanamu! Kwani wenye kukanusha hawana msaidizi wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anakiona kila kisichoonekana mbinguni na ardhini, na kwa hakika Yeye ni Mjuzi mno wa vilivyofichamana nyoyoni. Basi muogopeni Asiwaone mkiwa mko katika hali ya kudhamiria shaka au ushirikina katika kumpwekeshaYeye au juu ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukie, au muende kinyume na amri Yake katika mambo madogo ya hayo.
Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanya nyinyi, enyi watu, baadhi yenu washikilie nafasi ya wengine katika ardhi. Basi Mwenye kukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwenu madhara yake yatamrudia mwenyewe na ule ukafiri wake. Na hauwaongezei wakanushaji ule ukanushaji wao mbele ya Mola wao isipokuwa hasira na ghadhabu, na hakuwaongezei kule kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu isipokuwa upotevu na maangamivu.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Nipasheni habari: Ni kitu gani cha ardhi ambacho washirika wenu wamekiumba? Au hawa washirika wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wana ushirika na Mwenyezi Mungu katika uumbaji mbingu? Au tumewapa kitabu, hivyo basi wana ushahidi kutoka humo?» Lakini wakanushaji hawapeani ahadi isipokuwa udanganyifu na uhadazi.
Hakika Mwenyezi Mungu Anazizuia mbingu na ardhi siziondoke pale zilipo. Na lau zitaondoka pale zilipo, hakuna yoyote baada Yake Atakayezizuia. Mwenyezi Mungu ni Mpole katika kuahirisha mateso kwa makafiri na waasi, ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia dhambi zake na akarudi Kwake.
Na wakanushaji wa Kikureshi waliapa kwa Mwenyezi Mungu viapo vikali kwamba wakijiwa na mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu wa kuwaonya mateso ya Mwenyezi Mungu, watakuwa ni wenye kusimama wima zaidi na wenye kufuata haki zaidi kuliko Mayahudi, Wanaswara na wengineo. Na alipowajia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hilo halikuwaongezea wao isipokuwa kuwa mbali na haki na kuikimbia.
Kuapa kwao si kwa nia nzuri na kutafuta haki, isipokuwa huko ni kuwafanyia viumbe kiburi katika ardhi, wanakusudia kwa huko kuapa kufanya vitimbi vibaya, udanganyifu na ubatilifu. Na vitimbi vibaya haviwashukii isipokuwa wenyewe. Basi je, wana lolote la kunngojea, hao wenye kiburi na wenye vitimbi, isipokuwa ile adhabu iliyowashukia waliokuwa kama wao ambao waliwatangulia? Hutaupatia mpango wa Mwenyezi Mungu mabadiliko wala mageuko. Hakuna yoyote anayeweza kubadilisha wala kujiepusha na adhabu yeye mwenyewe wala mwingine.
Je, hawatembei makafiri wa Makkah kwenye ardhi, wakaona ulikuwa vipi mwisho wa wale waliokuwa kabla yao, kama vile 'Ād, Thamūd na mfano wao, na yale yaliyowapata ya maangamivu na yaliyowapata majumba yao ya uharibifu walipowakanusha Mitume, na makafiri hao walikuwa ni wakali zaidi na ni wenye nguvu zaidi kuliko makafiri wa Makkah? Na hakuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuna kitu chochote mbinguni wala ardhini chenye kumlemea na kumpita. Hakika Yeye ni Mjuzi sana wa matendo yao ni Mwenye uweza wa kuwaangamiza.
Na lau Mwenyezi Mungu Angaliwatesa watu kwa madhambi na maasia waliyoyatenda, Hangaliacha juu ya mgongo wa ardhi mnyama yoyote anayetembea juu yake. Lakini Anawapa muhula na Anachelewesha kuwaadhibu mpaka wakati maalumu Aliyoupanga. Na wakati wa kuwaadhibu ukija , basi Mwenyezi Mungu kwa waja Wake ni Mjuzi, hakuna yoyote kati yao atakayefichika Kwake, na hakuna chochote miongoni mwa mambo yao kilicho mbali na ujuzi Wake, na Atawalipa wao kwa walichotenda, chema au kibaya.