Tafsiri ya Sura Al-Isra'i kwa السواحلية kutoka Ali Muhsin Al - Swahili translation
Verse 1
Al-Isra'i
SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Verse 2
Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi!
Verse 3
Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani.
Verse 4
Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa.
Verse 5
Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo timizwa.
Verse 6
Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi.
Verse 7
Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.
Verse 8
Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri.
Verse 9
Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa.
Verse 10
Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.
Verse 11
Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa.
Verse 12
Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.
Verse 13
Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa.
Verse 14
Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu.
Verse 15
Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.
Verse 16
Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.
Verse 17
Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake.
Verse 18
Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa.
Verse 19
Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa.
Verse 20
Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki.
Verse 21
Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.
Verse 22
Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika.
Verse 23
Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.
Verse 24
Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.
Verse 25
Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake.
Verse 26
Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo.
Verse 27
Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.
Verse 28
Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini.
Verse 29
Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi.
Verse 30
Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona.
Verse 31
Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.
Verse 32
Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.
Verse 33
Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa.
Verse 34
Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa.
Verse 35
Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora.
Verse 36
Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa.
Verse 37
Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
Verse 38
Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi.
Verse 39
Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa.
Verse 40
Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa.
Verse 41
Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka. Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo.
Verse 42
Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi.
Verse 43
ﮋﮌﮍﮎﮏﮐ
ﮑ
Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu kabisa na hayo wanayo yasema.
Verse 44
Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira.
Verse 45
Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika.
Verse 46
Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao.
Verse 47
Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu aliye rogwa.
Verse 48
Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo hawawezi kuipata njia.
Verse 49
Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya?
Verse 50
ﭑﭒﭓﭔﭕﭖ
ﭗ
Sema: Kuweni hata mawe na chuma.
Verse 51
Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!
Verse 52
Siku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu.
Verse 53
Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.
Verse 54
Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao.
Verse 55
Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi.
Verse 56
Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine.
Verse 57
Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo.
Verse 58
Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu.
Verse 59
Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
Verse 60
Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
Verse 61
Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo?
Verse 62
Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu.
Verse 63
Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia.
Verse 64
Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.
Verse 65
Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
Verse 66
Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kukurehemuni nyinyi.
Verse 67
Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha.
Verse 68
Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate wa kumtegemea.
Verse 69
Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa kukunusuruni nasi.
Verse 70
Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.
Verse 71
Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
Verse 72
Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia.
Verse 73
Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki.
Verse 74
Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea kidogo.
Verse 75
Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi.
Verse 76
Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu.
Verse 77
Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu.
Verse 78
Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima.
Verse 79
Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.
Verse 80
Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie.
Verse 81
Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!
Verse 82
Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.
Verse 83
Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa.
Verse 84
Sema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu Mlezi anajua aliye ongoka katika njia.
Verse 85
Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.
Verse 86
Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia. Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya.
Verse 87
Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa.
Verse 88
Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.
Verse 89
Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.
Verse 90
Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii.
Verse 91
Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito kati yake ikimiminika.
Verse 92
Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso.
Verse 93
Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na Mtume?
Verse 94
Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume?
Verse 95
Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume wao.
Verse 96
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
Verse 97
Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.
Verse 98
Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya?
Verse 99
Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri.
Verse 100
Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo!
Verse 101
Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa!
Verse 102
Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia.
Verse 103
Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
Verse 104
Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.
Verse 105
Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.
Verse 106
Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.
Verse 107
Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.
Verse 108
Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe!
Verse 109
ﮃﮄﮅﮆﮇﮈ
ﮉ
Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu.
Verse 110
Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo.
Verse 111
Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa.
تقدم القراءة