Tafsiri ya Sura Ar-Rum kwa السواحلية kutoka Ali Muhsin Al - Swahili translation
Verse 1
ﮫ
ﮬ
Ar-Rum
Alif Lam Mim (A. L. M.)
Verse 2
ﮭﮮ
ﮯ
Warumi wameshindwa,
Verse 3
Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda
Verse 4
Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.
Verse 5
Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
Verse 6
Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui.
Verse 7
Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera.
Verse 8
Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.
Verse 9
Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao.
Verse 10
Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara.
Verse 11
Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake.
Verse 12
ﯝﯞﯟﯠﯡ
ﯢ
Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa.
Verse 13
Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao.
Verse 14
ﯭﯮﯯﯰﯱ
ﯲ
Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika.
Verse 15
Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika Bustani.
Verse 16
Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu.
Verse 17
ﭝﭞﭟﭠﭡﭢ
ﭣ
Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na asubuhi,
Verse 18
Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri.
Verse 19
Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa.
Verse 20
Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote.
Verse 21
Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Verse 22
Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi.
Verse 23
Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia.
Verse 24
Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia.
Verse 25
Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.
Verse 26
Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye.
Verse 27
Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Verse 28
Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili.
Verse 29
Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru.
Verse 30
Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.
Verse 31
Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina.
Verse 32
Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.
Verse 33
Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi,
Verse 34
Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
Verse 35
Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya ushirikina?
Verse 36
Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
Verse 37
Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
Verse 38
Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa.
Verse 39
Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa.
Verse 40
Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye.
Verse 41
Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.
Verse 42
Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa walio tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina.
Verse 43
Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana.
Verse 44
Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao.
Verse 45
Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri.
Verse 46
Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.
Verse 47
Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini.
Verse 48
Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha.
Verse 49
Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa.
Verse 50
Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Verse 51
Na tunge utuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wange endelea kukufuru.
Verse 52
Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi wakasikia wito wakisha geuka kukupa mgongo.
Verse 53
Wala wewe huwaongoi vipofu na upotovu wao. Huwasikilizishi ila wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea.
Verse 54
Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
Verse 55
Na siku itapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakipotozwa.
Verse 56
Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui.
Verse 57
Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala haitotakiwa toba yao.
Verse 58
Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote hapana shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si chochote ila ni waongo.
Verse 59
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za wasio jua.
Verse 60
Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala wasikupaparishe hao wasio kuwa na yakini.
تقدم القراءة