Tafsiri ya Sura Al'Anfal kwa السواحلية kutoka Ali Muhsin Al - Swahili translation
Verse 1
Al'Anfal
Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.
Verse 2
Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
Verse 3
ﭹﭺﭻﭼﭽﭾ
ﭿ
Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku.
Verse 4
Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira, na riziki bora, kwa Mola wao Mlezi.
Verse 5
Kama Mola wako Mlezi alivyo kutoa nyumbani kwako kwa Haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.
Verse 6
Wanajadiliana nawe kwa jambo la Haki baada ya kwisha bainika, kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti nao wanaona.
Verse 7
Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.
Verse 8
Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangachukia wakosefu.
Verse 9
Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana mfululizo.
Verse 10
Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
Verse 11
Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shet'ani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.
Verse 12
Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.
Verse 13
Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Verse 14
ﮱﯓﯔﯕﯖﯗ
ﯘ
Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto.
Verse 15
Enyi Mlio amini! Mkikutana na walio kufuru vitani msiwageuzie mgongo.
Verse 16
Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.
Verse 17
Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa, walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Msikizi na Mjuzi.
Verse 18
ﭩﭪﭫﭬﭭﭮ
ﭯ
Ndio hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya makafiri.
Verse 19
Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kujieni. Na mkiacha itakuwa ndio kheri kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea. Na jeshi lenu halitakufaeni kitu, japo likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini.
Verse 20
Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye, nanyi mnasikia.
Verse 21
Wala msiwe kama wale wanao sema: Tumesikia, na kumbe hawasikii.
Verse 22
Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni vile viziwi na bubu visio tumia akili zao.
Verse 23
Na Mwenyezi Mungu angeli jua wema wowote kwao ange wasikilizisha, na lau ange wasikilizisha wangeli geuka wakapuuza.
Verse 24
Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.
Verse 25
Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio dhulumu peke yao kati yenu. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Verse 26
Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, mkionekana wanyonge katika nchi, mnaogopa watu wasikunyakueni, naye akakupeni pahala pazuri pa kukaa, na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru.
Verse 27
Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua.
Verse 28
Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.
Verse 29
Enyi mlio amini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni kipambanuo, na atakufutieni makosa, na atakusameheni, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
Verse 30
Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.
Verse 31
Na wanapo somewa Aya zetu, wao husema: Tumesikia. Na lau tungeli penda tunge sema kama haya. Haya si chochote ila hadithi za watu wa kale tu.
Verse 32
Na walipo sema: Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni kweli itokayo kwako basi tunyeshee mawe kutoka mbinguni, au tuletee adhabu yoyote iliyo chungu.
Verse 33
Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu nawe umo pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba msamaha.
Verse 34
Lakini wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, na hali ya kuwa wanawazuilia watu Msikiti Mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake, bali walinzi wake hawakuwa ila wacha-Mngu tu. Lakini wengi katika wao hawajui.
Verse 35
Na haikuwa ibada yao kwenye hiyo Nyumba (Al Kaaba) ila ni kupiga miunzi na makofi. Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
Verse 36
Hakika wale walio kufuru hutoa mali yao ili kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao majuto, na kisha watashindwa. Na wale walio kufuru watakusanywa kwenye Jahannam.
Verse 37
Ili Mwenyezi Mungu apate kuwa pambanua walio waovu na walio wema, na kuwaweka waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika wote pamoja, na kuwatupa katika Jahannam. Hao ndio walio khasirika.
Verse 38
Waambie wale walio kufuru: Wakikoma watasamehewa yaliyo kwisha pita. Na wakiyarudia basi imekwisha pita mifano ya wa zamani.
Verse 39
Na piganeni nao mpaka isiwepo fitna na mateso, na Dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.
Verse 40
Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola Mwema na Msaidizi Mwema.
Verse 41
NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums (sehemu moja katika tano) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo yateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Verse 42
Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Verse 43
Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio vifuani.
Verse 44
Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu.
Verse 45
Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.
Verse 46
Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.
Verse 47
Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa fakhari na kujionyesha kwa watu, na wakawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka yote wanayo yafanya.
Verse 48
Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao, na akawaambia: Hapana watu wa kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipo onana majeshi mawili, akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja nanyi. Mimi naona msiyo yaona. Mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Verse 49
Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao: Watu hawa dini yao imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima.
Verse 50
Na laiti ungeli ona Malaika wanapo wafisha wale walio kufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni adhabu ya Moto!
Verse 51
Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa na mikono yenu, na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
Verse 52
Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao - walizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa sababu ya madhambi yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa kuadhibu.
Verse 53
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Verse 54
Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao - walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu.
Verse 55
Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao kufuru, basi hao hawaamini;
Verse 56
Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu.
Verse 57
Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili wapate kukumbuka.
Verse 58
Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini.
Verse 59
Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao wametangulia mbele. La, wao hawatashinda.
Verse 60
Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa.
Verse 61
Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Verse 62
Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa Waumini.
Verse 63
Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Verse 64
Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na Waumini walio kufuata.
Verse 65
Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani. Wakiwapo kati yenu ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu mia watawashinda elfu moja katika walio kufuru. Kwa sababu wao ni watu wasio fahamu.
Verse 66
Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa upo udhaifu kwenu. Kwa hivyo wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
Verse 67
Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
Verse 68
Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua.
Verse 69
Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Verse 70
Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi akiona kheri yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo chukuliwa kwenu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Verse 71
Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha mfanyia khiana Mwenyezi Mungu kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Verse 73
Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.
Verse 74
Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema.
Verse 75
Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
تقدم القراءة