Tafsiri ya Sura Al-Anbiya kwa السواحلية kutoka Ali Muhsin Al - Swahili translation
Verse 1
Al-Anbiya
IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza.
Verse 2
Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo.
Verse 3
Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona?
Verse 4
Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Verse 5
Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo.
Verse 6
Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa?
Verse 7
Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.
Verse 8
Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
Verse 9
Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka.
Verse 10
Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii?
Verse 11
Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine.
Verse 12
Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia.
Verse 13
Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa!
Verse 14
ﭯﭰﭱﭲﭳ
ﭴ
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu.
Verse 15
Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika.
Verse 16
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo.
Verse 17
Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo.
Verse 18
Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua.
Verse 19
Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
Verse 20
ﮰﮱﯓﯔﯕ
ﯖ
Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei.
Verse 21
Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua?
Verse 22
Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.
Verse 23
ﯮﯯﯰﯱﯲﯳ
ﯴ
Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo.
Verse 24
Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza.
Verse 25
Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
Verse 26
Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa.
Verse 27
ﭬﭭﭮﭯﭰﭱ
ﭲ
Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake.
Verse 28
Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.
Verse 29
Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu.
Verse 30
Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?
Verse 31
Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka.
Verse 32
Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake.
Verse 33
Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea.
Verse 34
Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele?
Verse 35
Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
Verse 36
Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema!
Verse 37
Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize.
Verse 38
Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
Verse 39
Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
Verse 40
Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula!
Verse 41
Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka.
Verse 42
Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
Verse 43
Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi!
Verse 44
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?
Verse 45
Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa.
Verse 46
Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu.
Verse 47
Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.
Verse 48
Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu,
Verse 49
Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama.
Verse 50
Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa?
Verse 51
Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua.
Verse 52
Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu?
Verse 53
ﯔﯕﯖﯗﯘ
ﯙ
Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
Verse 54
Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
Verse 55
Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu?
Verse 56
Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
Verse 57
Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu.
Verse 58
Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie.
Verse 59
Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu.
Verse 60
Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
Verse 61
Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia!
Verse 62
ﭴﭵﭶﭷﭸﭹ
ﭺ
Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim?
Verse 63
Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.
Verse 64
Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu!
Verse 65
Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi.
Verse 66
Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni?
Verse 67
Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
Verse 68
Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!
Verse 69
Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
Verse 70
ﯟﯠﯡﯢﯣ
ﯤ
Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.
Verse 71
Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
Verse 72
Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema.
Verse 73
Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
Verse 74
Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
Verse 75
Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema.
Verse 76
Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
Verse 77
Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
Verse 78
Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo.
Verse 79
Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
Verse 80
Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
Verse 81
Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.
Verse 82
Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
Verse 83
Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.
Verse 84
Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada.
Verse 85
Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri.
Verse 86
Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema.
Verse 87
Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
Verse 88
Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini.
Verse 89
Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi.
Verse 90
Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea.
Verse 91
Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
Verse 92
Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
Verse 93
Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu.
Verse 94
Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia.
Verse 95
Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea,
Verse 96
Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima;
Verse 97
Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
Verse 98
Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
Verse 99
Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo.
Verse 100
Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo).
Verse 101
Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo.
Verse 102
Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao.
Verse 103
Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa!
Verse 104
Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao.
Verse 105
Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.
Verse 106
ﮉﮊﮋﮌﮍﮎ
ﮏ
Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.
Verse 107
ﮐﮑﮒﮓﮔ
ﮕ
Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.
Verse 108
Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu?
Verse 109
Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa.
Verse 110
Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo.
Verse 111
Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
Verse 112
Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua.
تقدم القراءة