Tafsiri ya Sura Al-Mulk kwa السواحلية kutoka Ali Muhsin Al - Swahili translation
Verse 1
Al-Mulk
AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Verse 2
Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.
Verse 3
Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?
Verse 4
Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka.
Verse 5
Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu.
Verse 6
Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo!
Verse 7
Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka.
Verse 8
Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji?
Verse 9
Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa!
Verse 10
Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!
Verse 11
ﯷﯸﯹﯺﯻ
ﯼ
Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni!
Verse 12
Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa.
Verse 13
Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
Verse 14
Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?
Verse 15
Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa.
Verse 16
Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika!
Verse 17
Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu?
Verse 18
Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu?
Verse 19
Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu.
Verse 20
Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu.
Verse 21
Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki.
Verse 22
Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka?
Verse 23
Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu.
Verse 24
Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa.
Verse 25
Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?
Verse 26
Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha.
Verse 27
Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba.
Verse 28
Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu?
Verse 29
Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri.
Verse 30
Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika?
تقدم القراءة