ﰡ
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaapa kwa Malaika wanaojipanga, katika kuabudu kwao, mistari iliyofuatana na kushikana,
na kwa Malaika wanaofukuza mawingu na kuyaongoza kwa amri ya MwenyeziMungu,
na kwa Malaika wanaosoma utajo wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na maneno Yake,
kwamba muabudiwa wenu, enyi watu, ni Mmoja, Asiye na mshirika. Hivyo basi mtakasieni ibada na utiifu. Na Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Anachotaka miongoni mwa viumbe Vyake. Ama kiumbe, hafai kuapa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kwani kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina.
Yeye Ndiye Muumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili, na Ndiye Mpelekeshaji jua katika sehemu zake za kuchomozea na zile za kuchwea.
Sisi tumeupamba uwingu wa karibu kwa pambo la nyota.
Na tumeuhifadhi huo uwingu, kwa nyota, na kila shetani mwenye kuasi, mjeuri, aliyefukuzwa (kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu).
Hawawezi hao Mashetani kufika kwenye viumbe vya juu, navyo ni mbingu na Malaika waliyomo ndani yake, wakapata kuwasikiliza wanapoutamka wahyi ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anauleta, unaokusanya sheria Yake na makadirio Yake, na wanavurumizwa vimondo katika kila upande,
kwa kuwafukuza ili wasipate kusikiliza. Na huko kwenye Nyumba ya Akhera watakuwa na adhabu ya daima yenye kuumiza.
Isipokuwa yule aliyenyakuwa, miongoni mwa Mashetani, mnyakuo wa haraka, nao ni lile neno analolisikia mbinguni kwa haraka, akamtupia aliyekuwa chini yake, na yule mwingine akamtupia aliyekuwa chini yake. Basi pengine huenda akafikiwa na kimondo chenye kutoa mwangaza kabla hajalitupa, na pengine huwa amelitupa kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kabla ya kujiwa na kimondo kikamchoma, na yule mwingine akaenda nalo hadi kwa makuhani wakaongeza juu ya neno hilo maneno mia moja ya urongo.
Basi waulize, ewe Mtume, wenye kukanusha Kufufuliwa: Je kuumbwa kwao ni kugumu zaidi au ni hivyi viumbe tulivyoviumba? Kwa hakika, tulimuumba baba yao Ādam kwa udongo ulioshikana na kuambatana.
Bali ulistaajabu, ewe Mtume, kwa ukanushaji wao na kukataa kwao Kufufuliwa. Na la kustaajabiwa zaidi na lililo kubwa zaidi kuliko lile la kukataa kwao ni kwamba wao wanakucheza shere na kulidharau neno lako.
Na wanapokumbushwa walichokisahau au walichoghafilika nacho, hawanufaiki kwa huo ukumbusho wala hawazingatii.
Na wanapoiona miujiza yenye kutolea dalili unabii wako, wanakufanyia shere na wanastaajabu.
Na wanasema, «Halikuwa hili ulilotuletea isipokuwa ni uchawi uliojitokeza waziwazi.
Je, tunapokufa na tukawa ni mchanga na mifupa iliyochakaa, je sisi ni wenye kufufuliwa kutoka makaburini mwetu tukiwa hai?
au pia watafufuliwa baba zetu waliopita kabla yetu?»
Waambie, ewe Mtume, «Ndio mtafufuliwa hali mkiwa wanyonge, watwevu.»
Hakika ni kwamba huo utakuwa ni Mvuvio mmoja, wakitahamaki wao wamesimama kutoka makaburini mwao, wanatazama vituko vya Kiyama.
Na watasema, «Ewe maangamivu yetu! Hii ni siku ya kuhesabiwa na kulipwa!»
Hapo wataambiwa, «Hii ndiyo Siku ya Uamuzi wa haki baina ya viumbe, ambayo mlikuwa mkiikanusha duniani na mkiikataa.»
Na Malaika wataambiwa, «Wakusanyeni wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na wafananao na wao na waungu wao waliokuwa wakiwaabudu
badala ya Mwenyezi Mungu, na muwasukume kwa nguvu hadi kwenye moto wa Jahanamu.
«Na muwafunge kabla hawajafika kwenye moto wa Jahanamu, kwa kuwa wao ni wenye kuulizwa kuhusu matendo yao na maneno yao yaliyotokana na wao duniani, kwa namna ya kumshtukia kuwakaripia.»
Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Kwa nini hamsaidiani nyinyi kwa nyinyi?»
Bali wao Leo ni wenye kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, hawataenda kinyume nayo wala hawataepukana nayo, hawajisaidii wao wenyewe.
Na hapo makafiri watakabiliana wao kwa wao wakilaumiana na wakigombana.
Wafuasi watasema kuwaambia wafuatwa, «Nyinyi mlikuwa mkitujia kwa upande wa dini na haki, mkiifanya Sheria ni twevu kwetu, mkitutia chuki nayo na mkitupambia upotevu.»
Hapo watasema wafuatwa kuwaabia wafuasi, «Mambo si kama vile mnavyodai, bali ni nyoyo zenu zilikuwa zimekataa kuamini, zimeuelekea ukafiri na uasi.
«Na sisi hatukuwa na hoja juu yenu wala nguvu, tukaweza kwa hizo kuwazuilia kuamini. Bali nyinyi wenyewe, enyi washirikina, mlikuwa waasi wenye kupita mipaka ya haki.
«Hivyo basi ndio sisi sote ikalazimu tupate onyo la Mola wetu kuwa ni wenye kuonja adhabu, sisi na nyinyi, kwa yale tuliyoyatanguliza ya madhambi na maasia duniani.
« Ndipo tukawapoteza na njia ya Mwenyezi Mungu na ya kumuamini, kwa kuwa sisi wenyewe tulikuwa ni wapotevu kabla yenu. Na kwa hivyo tukapotea kwa sababu ya ukafiri wetu na tukawaangamiza nyinyi pamoja na sisi.»
Basi wafuasi na wafuatwa watashirikiana katika adhabu Siku ya Kiyama, kama walivyoshirikiana ulimwenguni katika kumuasi Mwenyezi Mungu.
Hivi ndivyo sisi tunavyowafanyia waliochagua mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu ulimwenguni na wakaacha kumtii, basi tutawaonjesha adhabu kali.
Hakika wale washirikina walikuwa duniani wakiambiwa, «Hapana mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu,» na wakaitwa kwenye mwito huo na wakaamrishwa kuyaacha yanayopingana nao, wanaufanyia kiburi na kumfanyia kiburi aliyekuja nao.
Na wanasema, «Je, tuache kuwaabudu waungu wetu kwa maneno ya mshairi mwenye wazimu?» wakimkusudia Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Wamesema urongo! Muhammad sivyo vile walivyomueleza. Bali amekuja na Qur’ani na upwekeshaji Mwenyezi Mungu, na akathibitisha ukweli wa Mitume katika kile walichokitolea habari kuhusu sheria ya Mwenyezi Mungu na kumpwekesha Yeye.
Hakika yenu nyinyi, enyi washirikina, kwa neno lenu, ukafiri wenu na kukanusha kwenu, ni wenye kuonja adhabu iliyo kali yenye uchungu.
Na hamtalipwa huko Akhera isipokuwa kwa lile la maasia mliokuwa mkilifanya duniani.
Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, waliomtakasia Ibada Yake, Akawatakasa na Akawahusu wao kwa rehema Yake, basi hao kwa hakika ni wenye kuokoka na adhabu yenye uchungu.
Hao waliotakaswa watapata riziki ijulikanayo isiyokatika ndani ya Pepo.
Riziki hiyo ni matunda aina mbalimbali. Na wao ni wenye kukirimiwa kwa takrima ya Mwenyezi Mungu
kuwafanyia wao ndani ya mabustani ya Pepo ya starehe ya milele.
Na miongoni mwa takrima yao watakayoipata kwa Mola wao, na kukirimiana wao kwa wao, ni kuwa wao watakuwa kwenye vitanda wameelekeana.
Zinazungushwa kwao gilasi za Pombe inayotoka kwenye mito inayotembea, hawachelei kuwa itamalizika,
ni nyeupe rangi yake, ni tamu katika kuinywa,
haina madhara yoyote ya akili wala ya mwili.
Na hapo kwao kwenye makao yao watakuwako wanawake waliojihifadhi, hawawatazami isipokuwa waume zao, wazuri wa macho,
kama kwamba wao ni mayai yaliyotunzwa ambayo hayajaguswa na mikono.
Hapo wataelekeana wakiulizana kuhusu hali zao za duniani na mambo ya usumbufu waliokuwa wakikutana nayo huko, na yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaneemesha nayo Peponi. Na huku ndiko kuliwazika kuliotimia.
Atasema msemaji miongoni mwa watu wa Peponi, «Kwa kweli, nilikuwa na rafiki duniani aliyeshikana na mimi.
«Aliyekuwa akisema, ‘Ni vipi wewe unaamini Ufufuzi ambao ni upeo wa kustaajabisha?
Je, tunapokufa, tukakatika vipande- vipande na tukawa mchanga na mifupa, kwani ni wenye kufufuliwa, kuhesabiwa na kulipwa kwa matendo yetu?’»
Atasema huyu Muumini aliyetiwa Peponi akiwaambia wenzake, «Je, nyinyi ni wenye kuchungulia mpate kuona mwisho wa yule rafiki?»
Hapo akachungulia na akamuona rafiki yake katikati ya Moto.
Muumini atasema kumwambia rafiki yake mwenye kukanusha kufufuliwa, «Ulikaribia kuniangamiza kwa kunizuia nisiamini lau nilikutii.
Na lau si wema wa Mola wangu kwa kuniongoza mimi kwenye Imani na kunithibitisha juu yake, ningalikuwa ni mwenye kuhudhurishwa kwenye adhabu pamoja na wewe.
«Je, ni kweli sisi ni wenye kukalishwa milele na kuneemeshwa, si wenye kufa
isipokuwa kifo chetu cha mwanzo huko ulimwenguni, na sisi si wenye kuadhibiwa baada ya kuingia kwetu Peponi?
Hakika starehe hii tuliyo nayo ndiyo kufaulu kukubwa.
«Basi kwa kupata mfano wa starehe hizi kamilifu, makazi ya daima na kufaulu kukubwa, na watende wenye kutenda duniani ili wazifikie huko Akhera.»
Je, hayo yaliyotangulia kuelezwa ya starehe za Pepo ni makaribisho bora na vipewa vya Mwenyezi Mungu, au ni mti mbaya uliolaaniwa wa zaqqūm, ambao ni chakula cha watu wa Motoni?
Sisi tumeufanya ni mtihani waliotahiniwa nao madhalimu kwa ukanushaji na kufanya mambo ya uasi na wakasema kwa njia ya kiburi, «Mtu wenu anawapa habari kwamba motoni kuna mti, na moto unakula miti.»
Hakika huo ni mti ambao unaota kwenye uketo wa moto wa Jahanamu, matunda yake yana sura mbaya
kama vichwa vya Mashetani.
Basi yanapokuwa hivyo, usiulize baada ya haya kuhusu utamu wake. Kwani washirikina ni wenye kula kutoka mti huo na ni wenye kujaza matumbo yao kwa matunda hayo.
Kisha wao, baada ya kuyala ni wenye kunywa kinywaji mchanganyiko kilicho kibaya na kilicho moto.
Kisha marejeo yao baada ya adhabu hii ni kuishia (hukohuko) kwenye adhabu ya Moto.
Hakika wao waliwakuta baba zao kwenye ushirikina na upotevu,
na wakakimbilia kuwafuata katika hilo.
na kwa hakika, kabla ya watu wako, ewe Mtume, walipotea na kuwa kando na haki ummah wengi waliotangulia.
Na kwa hakika, tuliwatumiliza kwa ummah hao Mitume waliowaonya adhabu, lakini wakakanusha.
Basi fikiria: ulikuwa vipi mwisho wa ummah hao walioonywa na wakakanusha? Waliadhibiwa na wakawa ni mazingatio kwa watu.
Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu Aliyowasafisha na Akawachagua kwa kuwapa rehema Yake kwa kule kumtakasa kwao Yeye.
Na kwa hakika Alituita kwa kutuomba Nabii wetu Nūḥ tumlinde na watu wake, basi bora wa wenye kumuitikia tulikuwa ni sisi.
Na tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na Waumini pamoja naye kutokana na maudhi ya washirikina na kutokana na kuzamishwa kwa mafuriko makubwa.
Na tukawafanya watoto wa Nūḥ ndio wenye kusalia baada ya kuzamishwa watu wake.
Na tukamuwekea utajo mwema na sifa nzuri kwa watu waliokuja baada yake wakawa wanamtaja nazo.
Amani imfikie Nūḥ na asalimike na kutajwa kwa ubaya katika kipindi cha watu wa mwisho, bali asifiwe na watu wa vizazi vinavyokuja baada yake.
Mfano wa malipo mema tuliomlipa Nūḥ, tutamlipa kila aliyefanya vizuri, miongoni mwa waja, katika kumtii Mwenyezi Mungu.
Hakika Nūḥ ni miongoni mwa waja wetu wenye kuamini, wenye kumtakasia Mwenyezi Mungu na wenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu kivitendo.
Kisha tukawazamisha wengine, wenye kukanusha kati ya watu wake, kwa mafuriko, kisisalie chochote, miongoni mwao, hata jicho lenye kupepesa.
Na miongoni mwa waliokuwa katika nyendo za Nūḥ, njia yake na mila yake ni Nabii wa Mwenyezi Mungu Ibrāhīm,
alipomjia Mola wake kwa moyo uliyojitenga na kila itikadi ya ubatilifu na tabia ya kujitukanisha,
alipomwambia babake na watu wake kwa njia ya kuwakanya, «Ni kitu gani hiko mnachokiabudu badala ya Mwenyezi Mungu?
Je, mnataka kuabudu waungu wa kuzuliwa na mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake?
Mnamdhani Mola wa viumbe vyote Atawafanya nini mkimshirikisha Yeye na mkamuabudu asiyekuwa Yeye?
Akatazama mtazamo mmoja kwenye nyota kulingana na mila ya watu wake kuhusu hilo, huku akifikiria udhuru wa kuutoa ili asipate kutoka na wao kwenda kwenye sherehe zao,
akawaambia, «Mimi ni mgonjwa.» Hii ilikuwa ni ishara ya mbali kutoka kwake.
Basi wakamuacha nyuma yao.
Akabeta kwa haraka kuelekea kwenye masanamu wa watu wake, akasema kwa njia ya kuwakejeli, «Si mkile chakula hiki ambacho washika mlango wenu wanawapatia?
Muna nini nyinyi mbona hamsemi wala hamumjibu mwenye kuwaomba?
Akawaelekea waungu wao kuwapiga na kuwavunja-vunja kwa mkono wake wa kulia, ili kuwathibitishia makosa ya kuwaabudu.
Wakaja kumkabili kwa haraka na mbio huku wana hasira.
Ibrāhīm akakutana na wao akiwa imara kwa kusema, «Vipi mtaabudu masanamu mnaowachonga nyinyi wenyewe na mnaowatengeneza kwa mikono yenu,
na mnaacha kumuabudu Mola wenu Aliyewaumba nyinyi na Akayaumba matendo yenu?»
Hoja ilipowasimamia, waliamua kutumia nguvu na wakasema, «Jengeni jengo kwa ajili yake, mlijaze kuni kisha mumtupe ndani yake»
Watu wa Ibrāhīm wakataka kumfanyia vitimbi ili wamuangamize, tukawafanya wao kuwa ndio wenye kutendeshwa nguvu na kushindwa. Mwenyezi Mungu Akavirudisha vitimbi vyao kwenye shingo zao na akaufanya ule moto uwe baridi na salama kwa Ibrāhīm.
Akasema Ibrāhīm, «Mimi nahamia kwa Mola wangu kutoka kwenye mji wa watu wangu kuelekea pale ambapo nitamakinika kumuabudu Mola wangu, kwani Yeye Atanielekeza kwenye kheri ya Dini yangu na dunia yangu.
Mola wangu! Nipe mtoto mwema.»
Tukamkubalia ombi lake na tukambashiria kuwa atapata mtoto wa kiume atakayekuwa mpole ukubwani mwake, naye ni Ismā'īl.
Alipokuwa mkubwa Ismā'īl, akawa anatembea na babake, babake alimwambia, «Mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja, je, una maoni gani?» (na ndoto za Manabii ni za kweli). Ismā'īl akasema, kwa kumridhisha Mola wake, kumtii mzazi wake na kumsaidia juu ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, «Endelea katika jambo Alilokuamrisha Mwenyezi Mungu la kunichinja mimi. Utanikuta, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni mvumilivu, mtiifu na ni mwenye kutarajia malipo mema (kutoka kwa Mwenyezi Mungu)».
Walipojisalimisha wao wawili kwa kuifuata amri ya Mwenyezi Mungu na kuiandama, na Ibrāhīm akambwaga Ismā'īl chini, kwa upande wa paji la uso, ili kumchinja.
Na tukamuita Ibrāhīm katika hali hiyo ngumu kwamba: Ewe Ibrāhīm! Umeshalifanya uliloamrishwa na, kwa hivyo,
umeisadikisha ndoto yako. Hakika yetu sisi kama vile tulivyokulipa mema kwa kuamini kwako , ndivyo tunavyowalipa wale waliofanya wema mfano wako, tuwaepushie shida duniani na Akhera.
Hakika amri ya kuwa wewe umuue mwano ndio mtihani mgumu uliodhihirisha ukweli wa Imani yako.
Na tukamuokoa Ismā'īl, na tukamuekea kondoo mkubwa kuwa ni badala yake.
Na tukambakishia Ibrāhīm baada yake sifa njema kwa watu.
Maamkizi kwa Ibrāhīm kutoka kwa Mola wake na kumuombea asalimike na kila dhara.
Kama tulivyomlipa malipo mema Ibrāhīm kwa utiifu wake kwetu na kufuata kwake amri yetu, ndivyo tutakavyowalipa wenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu.
Hakika yeye ni miongoni mwa waja wetu Waumini waliyoipa hiyo sifa ya uja haki yake.
Na tukampa bishara Ibrāhīm ya mtoto wake, Isḥāq, kuwa atakuwa Nabii, miongoni mwa watu wema. Hayo yakiwa ni malipo ya uvumilivu wake na kuridhika kwake na amri ya Mola wake na utiifu wake Kwake.
Na tukawateremshia baraka. Na miongoni mwa wale wanaotokana na kizazi chao kuna anayemtii Mola wake, anayeifanyia wema nafsi yake, na kuna anayeidhulumu (nafsi yake) dhulma iliyo wazi kwa ukafiri wake na utendaji wake maasia.
Na kwa hakika tuliwafanyia wema Mūsā na Hārūn kwa kuwapa unabii na utume.
Na tukawaokoa wao wawili na watu wao kutokana na gharika, utumwa na unyonge waliokuwa nao.
Na tukawanusuru, wakawa na enzi, usaidizi na ushindi juu ya Fir'awn na jamaa zake.
Na tukawapa wao wawili Taurati yenye ufafanuzi,
na tukawaongoza njia iliyonyoka isiyokuwa na upotovu, nayo ni Uislamu, Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo Amewatumiliza Manabii Wake kwayo,
na tukazifanya sifa zao nzuri na utajo wao mwema ni vyenye kusalia baada yao.
Maamkizi kwa Mūsā na Hārūn kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sifa njema na kuwaombea wao wasalimike na kila dhara.
Kama tulivyowalipa wao malipo mema , ndivyo tutakavyowalipa wenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu wenye kututakasia kwa ukweli, kuamini na kutenda.
Hakika ya wao wawili ni miongoni mwa waja wetu waliojikita katika Imani.
Na hakika mja wetu Ilyas ni miongoni mwa wale ambao tuliwakirimu kwa unabii na utume.
Kumbuka na utaja pindi aliposema kuwaambia watu wake, kati ya Wana wa Isrāīl, «Mcheni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na mumuogope, na msimshirikishe mwengine pamoja na Yeye.
Vipi nyinyi mtaliabudu sanamu ambalo ni kiumbe dhaifu na mtamuacha Mzuri wa kuumba, Mwenye sifa nzuri na kamilifu kabisa,
mkawa hamtamuabudu Mwenyezi Mungu Ambaye ni Mola wenu Aliyewaumba nyinyi na Akawaumba baba zenu waliopita kabla yenu?»
Watu wa Ilyas walimkanusha Nabii wao. Basi Mwenyezi Mungu , kwa hakika, Atawakusanya Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na wateswe.
Isipokuwa wale waja wa Mwenyezi Mungu waliomtakasia Mwenyezi Mungu Dini yao, basi hao ni wenye kuokoka na adhabu Yake.
Tulimfanya Ilyas awe na sifa nzuri kwa ummah waliokuja baada yake.
Maamkizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na sifa njema kwa Ilyas.
Na kama tulivyomlipa Ilyas malipo mema kwa utiifu wake, ndivyo tutakavyowalipa walio wema miongoni mwa waja wetu Waumini.
Hakika yake yeye ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu waliomtakasia wenye kufuata amri zake kivitendo.
Na hakika mja wetu Lūṭ tulimchagua na tukamfanya ni miongoni mwa Mitume.
Tulipomuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake wote,
isipokuwa mkongwe aliyezeeka, naye ni mke wake, ambaye aliangamia pamoja na wale walioangamia miongoni mwa watu wake kwa ukafiri wake.
Kisha tukawaangamiza wakanushaji waliosalia miongoni mwa watu wake.
Na hakika yenu nyinyi, enyi watu wa Makkah mnazipitia katika safari zenu nyumba za watu wa Lūṭ na athari zao katika kipindi cha asubuhi,
na pia mnazipitia katika kipindi cha usiku. Basi hamtii akilini, mkaogopa kisije kikawafika nyinyi kile kilichowafika wao?
Hakika mja wetu Yūnus, tulimchagua na tukamfanya ni miongoni mwa Mitume.
Alipokimbia kutoka mji wake, akiwa na hasira juu ya watu wake, akapanda jahazi iliyojaa abiria na vyombo.
Mawimbi makubwa yakaizunguka jahazi hiyo kila upande. Na watu waliokuwa wamepanda jahazi wakapiga kura ili kupunguza shehena ili wasizame. Yūnus akawa ni miongoni mwa wale walioshindwa kwa kura.
Hivyo basi akatupwa baharini na chewa akammeza, na hali ni kwamba Yūnus, amani imshukie, ameleta jambo la kumfanya alaumiwe.
Lau si yale yaliyotangulia kwake, ya wingi wa Ibada na matendo mema kabla ya kuingia ndani ya tumbo la chewa kwa kusema, «Hapana Mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa wewe, kutakasika na sifa za upungufu ni kwako, mimi nimekuwa miongoni mwa wenye kudhulumu,»
angalikaa ndani ya tumbo la chewa, na lingalikuwa ni kaburi lake mpaka Siku ya Kiyama.
Tukamtoa kwenye tumbo la chewa na tukamtupa kwenye ardhi tupu, isiyokuwa na miti wala majengo, akiwa dhaifu wa mwili.
Na tukamuoteshea mmea wa matango ili umfinike na anufaike nao.
Tukamtumiliza aende kwa watu wake wanaofikia elfu mia moja, bali wanazidi idadi hiyo.
Wakamuamini na wakafuata aliyokuja nayo kivitendo, na kwa hivyo tukawastarehesha maishani mwao mpaka wakati wa kufika ajali zao.
Basi waulize watu wako, ewe Mtume, «Ni vipi wamemfanya Mwenyezi Mungu ana watoto wa kike ambao wao wenyewe wanawachukia, na wao wana watoto wa kiume wanaowataka?»
Na waulize wao, «Je, tuliwaumba Malaika wakiwa wanawake, na hali wao wapo (wakishuhudia uumbaji huo)?»
Na miongoni mwa urongo wao ni kule kusema kwao, «Mwenyezi Mungu Amezaa!
Na kwa hakika, wao ni warongo, kwa kuwa wanakisema wasichokijua.»
Ni kwa kitu gani Mwenyezi Mungu Achague watoto wa kike na sio wa kiume?
Ni uamuzi mbaya sana mnaoutoa, enyi watu, wa kuwa Mwenyezi Mungu Ana watoto wa kike na nyinyi mna watoto wa kiume, na hali nyinyi hamridhiki nafsi zenu kuwa na watoto wa kike.
Je, hamkumbuki kwamba haifai wala haitakikani Awe na mtoto? Ametukuka Mwenyezi Mungu na kuwa mbali na hilo, umbali ulio juu sana.
Lakini je, mna hoja ya wazi juu ya hilo neno lenu na uzushi wenu?
Iwapo mna hoja ndani ya kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, basi kileteni, mkiwa ni wa kweli katika hilo neno lenu.
Na washirikina walifanya kuwa kuna uhusiano wa kizazi baina ya Mwenyezi Mungu na Malaika, na hakika ni kwamba Malaika washajua kuwa washirikina ni wenye kuletwa Siku ya Kiyama ili kuadhibiwa.
Ametakasika Mwenyezi Mungu na kila lisilofaa asifike nalo miongoni mwa yale wanaomsifu nayo washirikina.
Lakini wale waja wa Mwenyezi Mungu wanaomtakasia katika kumuabudu hawamsifu isipokuwa kwa sifa zinazolingana na utukufu Wake, kutakasika ni Kwake.
Hakika yenu nyinyi, enyi wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na kile mnachokiabudu badala ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa waungu,
hamkuwa ni wenye kumpoteza yoyote
isipokuwa yule Aliyemkadiria Mwenyezi Mungu aingie kwenye Moto wa Jaḥīm kwa sababu ya ukafiri wake na udhalimu wake.
Malaika wanasema, «Hakuna yoyote miongoni mwetu isipokuwa ana makao maalumu mbinguni.
Na sisi ndio tunaosimama kwa kujipanga kwa safu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtii.
Na sisi ndio tunaomtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisichofaa kunasibishwa nacho.»
Na hakika makafiri wa Makkah walikuwa wakisema kabla hujatumilizwa,
«Ewe Mtume! Lau vingalitujia vitabu na Manabii vile vilivyowajia wa mwanzo kabla yetu,
tungalikuwa waja wa Mwenyezi Mungu wakweli katika Imani, waliotakaswa kwa kufanya Ibada.»
Ulipowajia wao utajo wa watu wa mwanzo na utajo wa watu wa mwisho na kitabu kikamilifu kabisa na bora wa Mitume, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, walimkanusha. Basi wataijua adhabu watakayopatiwa Siku ya Mwisho.
Kwa hakika lishatangulia neno letu, ambalo halina namna ya kurudi, la kuwaahidi waja wetu waliopewa utume
kwamba watapata usaidizi juu ya maadui zao, kwa hoja na nguvu,
na kwamba askari wetu wanaopigana jihadi katika njia yetu ndio wenye kuwashinda maadui zao kila mahali, kuzingatia mwishoni na marejeo.
Basi wape mgongo, ewe Mtume, wale walioshindana na wasiikubali haki mpaka ukamalizika muda waliopatiwa muhula na ikaja amri ya Mwenyezi Mungu ya wao kuadhibiwa,
wangojee na subiri uone: ni adhabu gani itakayowashukia wao kwa kuenda kinyume nawe? Basi wataiona adhabu ya Mwenyezi Mungu itakayowashukia.
Je kuteremkiwa kwao na adhabu yetu ndilo jambo wanalokuharakishia, ewe Mtume?
Basi adhabu yetu itakapowashukia, asubuhi mbaya zaidi ni asubuhi yao!
Na uwape mgongo mpaka Mwenyezi Mungu Atoe idhini ya wao kuadhibiwa.
Na uwangojee, kwani wataiona adhabu itakayowashukia na mateso.
Mola wa enzi na utukufu Ameepukana na kuwa juu ya kila kile ambacho wanaomzulia urongo wanamsifu nacho.
Na maamkizi ya Mwenyezi Mungu ya daima,sifa Zake na amani Yake ziwafikie Mitume wote.
Na shukrani na sifa njema ni za Mola wa viumbe wote ulimwenguni na Akhera. Yeye Ndiye Mstahiki wa hilo Peke Yake, Hana mshirika Wake.