ﰡ
Ṭā, Sīn, Mīm. (Yametangulia maelezo kuhusu herufi ziliokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah).
Hizi ni aya za Qur’ani niliyokuteremshia, ewe Mtume, yenye kufafanua kila kile ambacho waja wanakihitajia katika ulimwengu wao na Akhera yao.
Tunakusimulia wewe habari ya Mūsā na Fir’awn kwa ukweli (ili wazingatie wale) watu wanaoiamini hii Qur’ani na wakubali kwamba inatoka kwa Mwenyezi Mungu na wafanye matendo yanayoambatana na uongofu wake.
Hakika Fir’awn alifanya kiburi na akapita mipaka katika nchi, akawafanya watu wake kuwa ni makundi tafauti-tafauti, akawa analinyongesha kundi moja ya hayo, nalo ni lile la Wana wa Isrāīl, akawa anawaua watoto wao wa kiume na anawabakisha wanawake wao kwa kutumika na kudharauliwa, Hakika yeye alikuwa ni miongoni mwa waharibifu katika ardhi.
Na tunataka kuwafadhili wale ambao Fir'awn aliwafanya wanyonge nchini, tuwafanye ni viongozi katika wema na ni wenye kuulingania, na tuwafanye wao wairithi nchi baada ya kuangamia Fir'awn na watu wake.
Na tuwape uthabiti katika nchi na tumfanye Fir’awn, Hāmān na askari wao waone, kutoka kundi hili linalonyongeshwa kile walichokuwa wakikiogopa cha kuangamia kwao na kuondoka ufalme wao na kuwatoa wao kwenye nyumba zao kwa mkono wa mzaliwa wa Wana wa Isrāīl.
Na tukampa mawazo mamake Mūsā alipomzaa na akamuogopea asije Fir'awn akamchinja kama anavyowachinja watoto wa wana wa Isrāīl kwamba «mnyonyeshe ukiwa mtulivu, na pindi uogopapo kujulikana mambo yake, muweke sandukuni na ulitupe kwenye mto wa Nail bila ya kuogopa kwamba fir'awn na watu wake watamuua na bila ya kuwa na masikitiko ya kuepukana na yeye, hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamtumiliza kuwa Mtume.»
Hapo akamuweka sandukuni na akalitupa kwenye mto wa Nail, na wafuasi wa Fir'awn wakalipata na wakalichukua, na mwisho wake ukawa vile Alivyokadiria Mwenyezi Mungu kuwa Mūsā awe ni adui yao kwa kuwa kinyume na dini yao, na awatie kwenye huzuni ya kuzamishwa na kuondokewa na ufalme wao mikononi mwake. Kwa hakika, Fir'awn na Hāmān na wasaidizi wao walikuwa wafanyaji makosa washirikina.
Na mke wa Fir'awn alipomuona , Mwenyezi Mungu Alimtia mapenzi moyoni mwake na akasema kumwambia Fir'awn, «Mtoto huyu atakuwa chimbuko la furaha kwangu mimi na wewe, Msimuue kwani huenda tukapata kheri kutoka kwake au tumfanye ni mtoto wetu» na hali Fir'awn na jamaa wa nyumbani kwake hawafahamu kwamba maangamivu yao yatatokana mikononi mwake.
Na kifua cha mamake Mūsā kikawa hakijishughulishi na kitu chochote duniani isipokuwa hamu ya Mūsā na kumtaja, na alikaribia kudhihirisha kuwa yule ni mwanawe lau si sisi kumthibitisha, naye akavumilia asilidhihirishe hilo, ili awe ni miongoni mwa wenye kuamini ahadi ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuwa na yakini nayo.
Na akasema mamake Mūsā kumwambia nduguye wa kike alipomtupa mtoni, «Fuata athari za Mūsā uone atafanywa nini? Akafuata athari zake na akamuona kwa mbali na hali watu Fir'awn hawajui kwamba yeye ni dadake na kwamba yeye afuatilia habari zake.
Na tulimzuia Mūsā asinyonye kutoka kwa wanyonyeshaji kabla hatujamrudisha kwa mamake, hapo dadake akasema, «Je, ni waonyeshe watu wa nyumba ambao watamlea na kumnyonyesha vizuri na ambao watakuwa na huruma naye? Wakamkubalia hilo.
Basi tukamrudisha Mūsā kwa mamake, ili jicho lake litulie kwake na tukamtekelezea ahadi yetu kwake, kwa kuwa alirudi kwake akiwa amesalimika na kuuawa na Fir'awn, na ili asihuzunike kwa kuepukana naye, na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, ile Aliyowaahidi kuwa atawarudishia na Amfanye ni miongoni mwa Mitume. Hakika Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake, lakini wengi wa washirikina hawajui kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli.
Na Alipofikia Mūsā umri wa kuwa na nguvu na ikakamilika akili yake, tulimpa busara na elimu ya kujulia hukumu za Sheria. Na kama tulivyompa Mūsā malipo mema kwa utiifu wake na wema wake, tunampa malipo mema mwenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu.
Na Mūsā aliingia mjini kwa kujificha wakati ambapo watu wake walikuwa wako katika hali ya kughafilika, akawapata humo watu wawili wanapigana, mmoja wao ni katika wana wa Isrāīl jamaa za Mūsā na mwingine ni katika jamaa za Fir’awn. Basi yule aliyekuwa ni katika jamaa ya Mūsā alitaka msaada dhidi ya yule Aliyekuwa katika maadui zake, hapo Mūsā akampiga kofi na akafa. Mūsā akasema alipomuua, «Huu ni katika ushawishi wa Shetani aliyenipandisha hasira zangu mpaka nikampiga huyu akafa. Hakika ya Shetani ni adui ya mwanadamu ni mwenye kupoteza njia ya uongofu, ni mwenye uadui wa waziwazi.» Kitendo hiki cha Mūsā kilikuwa kabla ya kupewa unabii.
Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa kumuua mtu ambaye hukuniamuru kumuua, basi nisamehe dhambi hilo.» Na Mwenyezi Mungu Akamsamehe. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe sana dhambi za waja Wake, ni Mwenye huruma nao sana.
Mūsā akasema, «Mola wangu! Kwa vile ulivyonineemesha kwa toba, msamaha na neema nyingi, sitakuwa mwenye kumsaidia yoyote kufanya uasi wake na uhalifu wake.
Hivyo basi Mūsā akaingiwa na kicho akiwa kwenye mji wa Fir’awn, anatafuta habari zinazozungumzwa na watu kuhusu yeye na yule mtu aliyemuua, hapo akamuona yule mtu wake wa jana akipigana na Mmisri mwingine na akimtaka amsaidie. Mūsā alimwambia, «Kwa kweli, wewe ni mwingi wa upotofu, ni mpotevu waziwazi.»
Basi alipotaka Mūsā kumshika Mmisri kupambana naye, alisema, «Je, unataka kuniua mimi kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki isipokuwa kuwa jeuri katika nchi, na hutaki kuwa ni miongoni mwa wale wanaofanya upatanishi kati ya watu.»
Na akaja mtu mbiombio kutoka mwisho wa mji, akasema, «Ewe Mūsā! Kwa hakika wale watukufu wa jamii ya Fir’awn wanafanya njama ya kukuua na wanashauriana juu ya hilo, basi toka. Kwani mimi ni kati ya wale wanaokupa ushauri mzuri na wanaokupendelea wema.»
Hapo Mūsā akautoka mji wa Fir'awn akiwa katika hali ya kuogopa, akitazamia kukamatwa na wale wanaomtafuta, na akamuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe na watu madhalimu.
Na alipokusudia kuelekea nchi ya Madyan, na akatoka nje ya utawala wa Fir'awn, alisema, «Nina matumaini kwamba Mola wangu Ataniongoza njia nzuri ya kuelekea Madyan.»
Alipoyafikia maji ya Madyan, alilikuta hapo kundi la watu wanawapa maji wanyama wao, na akawakuta, kando ya kundi hilo, wanawake wawili wamejitenga na watu na wamewazuilia wanyama wao na pale penye maji, kwa kushindwa kwao na udhaifu wao wa kutoweza kubanana na wanaume, na wanangojea mpaka wanyama wa watu waondoke kwenye maji kisha hapo wawapatie wanyama wao maji. Mūsā, amani imshukiye, alipowaona aliwaonea huruma, kisha alisema kuwaambia, «Muna nini nyinyi?» wakasema, «Hatuwezi kubanana na wanaume, na hatuchoti maji mpaka watu wamalize kuchota, na baba yetu ni mzee sana hawezi kuwachotea maji wanyama wake kwa udhaifu wake na uzee wake.»
Basi Mūsā akawachotea maji wanyama wa wale wanawake wawili, kisha akageuka kwenda kwenye kivuli cha mti kujifinika nacho na akasema, «Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa wema wako wowote ule utakaoniletea,» kama vile chakula. Na njaa ilikuwa imemshika sana.
Hapo akaja mmoja wa wale wanawake wawili aliyewachotea maji akitembea na huku yuwaona haya akasema, «Baba yangu anakuita ili akupe malipo ya maji uliyotuchotea.» Na Mūsā akaenda na yeye hadi kwa baba yake. Alipomjia baba yake na akamsimulia habari zake yeye pamoja na Fir’awn na watu wake, yule baba wa mwanamke alisema, «Usiogope! Umeokoka na watu madhalimu, nao ni Fir'awn na watu wake, kwani wao hawana mamlaka yoyote nchini kwetu.»
Akasema mmoja wa wanawake wawili kumwambia baba yake, «Ewe baba yangu! Muajiri yeye akuchungie wanyama wako, kwani mtu bora wa wewe kumuajiri kwa kuchunga ni yule aliye na nguvu ya kuwalinda wanyama wako, aliye muaminifu ambaye huchelei kuwa atakufanyia hiana katika amana unayompatia.»
Mzee akasema kumwambia Mūsā, «Mimi nataka kukuoza mmoja wa mabinti wangu hawa wawili, kwa sharti uwe muajiriwa wangu wa kuwachunga wanyama wangu kwa kipindi cha miaka minane. Na ukikamilisha miaka kumi, basi hiyo ni hisani yako. Na mimi sitaki kukusumbua kwa kuifanya miaka kumi. Utanikuta mimi, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni miongoni mwa watu wema, katika uzuri wa tangamano na utekelezaji ahadi wa ninayoyasema.
Mūsā akasema, «Hilo ulilolisema lisimame kuwa ndio ahadi baina yangu mimi na wewe, muda wowote wa vipindi viwili nitakaa kazini, nitakuwa nimekutekelezea, na sitatakiwa kuengeza juu yake, na Mwenyezi Mungu, kwa tunayoyasema, ni Mtegemewa, ni Mtunzi, Anatuona na Anakijua kile tulichofanya mapatano juu yake.»
Basi Nabii wa Mwenyezi Mungu Mūsā, amani imshukiye, alipomtekelezea mwenzake kipindi cha miaka kumi, nao ni muda mkamilifu zaidi wa vile vipindi viwili, na akaenda na watu wa nyumbani kwake kuelekea Misri, aliona moto upande wa jabali la Ṭūr. Mūsā alisema kuwaambia watu wa nyumbani kwake, «Subirini na mngojee. Mimi nimeona moto. Huenda nikawaletea habari kutoka kule, au nikawaletea kinga cha moto mkapata kujiotesha nacho.»
Basi Mūsā alipoujia moto, Mwenyezi Mungu Alimuita kutoka upande wa bonde la mkono wa kulia wa Mūsā, katika ardhi iliyobarikiwa ya upande wa mti kwamba: «Ewe Mūsā! Mimi Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote,»
na kwamba: «itupe fimbo yako!» Na Mūsā akaitupa, ikageuka kuwa nyoka anayetembea kwa haraka. Alipoiona inatetemeka kama kwamba ni nyoka kama walivyo nyoka wengine, aligeuka kumkimbia na asizunguke kwa kuogopa. Na hapo Mola wake Alimuita, «Ewe Mūsā! Nielekee mimi, na usiogope! Wewe ni miongoni mwa wenye kuaminika na kila lenye kuchukiza.
«Tia mkono wako kwenye uwazi wa kanzu yako uliofunguliwa kifuani na uutoe, utatoka kuwa mweupe, kama barafu, ambao si wa ugonjwa wala mbalanga, na ujikumbatie kwa mikono yako ili usalimike na kicho. Hivi viwili nilivyokuonesha, ewe Mūsā, vya fimbo kugeuka nyoka na kuufanya mkono wako kuwa mweupe na wenye kung’ara, si kwa ugonjwa wala mbalanga, ni dalili mbili kutoka kwa Mola wako, uende nazo kwa Fir’awn na watukufu wa watu wake.» Hakika Fir’awn na viongozi walio karibu naye walikuwa ni wakanushaji.
Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimemuua mtu wa jamii ya Fir’awn, basi naogopa wasije wakaniua.
Na ndugu yangu, Hārūn, ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi, basi mtume yeye pamoja na mimi awe msaidizi wangu, ataniamini na atawafafanulia wao yale ninayowaambia. Mimi ninachelea wasije wakanikanusha mimi kwa maneno yangu nitakayowaambia kwamba mimi nimetumilizwa kwao.»
Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Tutakupa nguvu kwa ndugu yako, na tutawapa nyinyi wawili hoja juu ya Fir’awn na watu wake wasiweze kuwafikia nyinyi kwa ubaya wowote. Nyinyi wawili na wale wenye kuwaamini nyinyi ndio mtakaopewa ushindi juu ya Fir’awn na watu wake kwa sababu ya aya zetu na ukweli unaoonyeshwa na hizo aya.»
Mūsā alipomjia Fir’awn na viongozi wa mamlaka yake na aya zetu na hoja zetu zenye kushuhudilia ukweli wa yale aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake, walimwambia Mūsā, «Hili ulilotujia nalo si chochote isipokuwa ni uchawi uliouzua kwa urongo na ubatilifu. Na hatujawahi kusikia jambo hili unalotuitia kwalo kutoka kwa wale waliotutangulia waliopita kabla yetu.»
Na Mūsā alisema kumwambia Fir’awn, «Mola wangu Anamjua zaidi aliye kwenye sawa kati yetu, aliyekuja na uongofu kutoka Kwake, na yule atakayekuwa na mwisho wa kushukuriwa katika Nyumba ya Akhera. Kwa hakika, madhalimu hawatayapata matakwa yao.»
Na Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, «Enyi viongozi! Mimi sijui kwamba nyinyi muna mola isipokuwa mimi anayestahiki kuabudiwa. Basi, ewe Hāmān! Niwashie moto juu ya udongo mpaka ushikane, na unijengee jengo lenye urefu wa kuelekea juu, kwani huenda nikamchungulia muabudiwa wa Mūsā ambaye yeye anamuabudu na anawaita watu wamuabudu. Na mimi ninadhani kuwa yeye ni miongoni mwa warongo katika hayo anayoyasema.»
Na Fir’awn na askari wake walifanya kiburi katika nchi ya Misri bila ya haki kwa kukataa kumuamini Mūsā na kumfuata katika lile alilowaitia na wakadhani kwamba baada ya kufa kwao hawatafufuliwa.
Tukamchukua Fir’awn na askari wake tukawatupa wote baharini na tukawazamisha. Basi angalia, ewe Mtume, ulikuwa vipi mwisho wa hawa waliojidhulumu wenyewe wakamkanusha Mola wao?
Na tumemfanya Fir’awn na watu wake ni wenye kuongoza kwenye njia ya motoni, wakifuatwa na watu wa ukafiri na uasi. Na Siku ya Kiyama hawataokolewa. Hiyo ni kwa sababu ya ukafiri wao na kuwakanusha kwao Mitume wa Mola wao na kuendelea kwao kufanya hivyo.
Na tukamfuatilizia Fir’awn na watu wake laana na hasira kutoka kwetu juu yao. Na Siku ya Kiyama, wao watakuwa ni miongoni mwa wale ambao matendo yao yalikuwa yamechafuka, wale watakaowekwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Na hakika tulimpa Mūsā Taurati baada ya kuwaangamiza ummah waliokuwa kabla yake, kama vile watu wa Nūḥ, ‘Ād, Thamūd, na watu wa Lūṭ na watu wa Madyan, hali ya kuwa Taurati ina hoja kwa Wana wa Isrāīl ambazo kwa hizo wanayaona yale yanayowafaa na yanayowadhuru, na ndani yake kuna rehema kwa wanaoifuata Taurati kivitendo. Huenda wao wakazikumbuka neema za Mweyezi Mungu juu yao, wakamshukuru kwa hizo na wasimkanushe.
Na hukuwako, ewe Mtume, upande wa jabali la jua la kuchwa wa Mūsā, tulipombebesha maamrisho yetu na makatazo yetu, na hukuwa ni kati ya wale waliolishuhudia hilo mpaka kusemwe kwamba habari hii imekufikia kwa njia hii.
Lakini sisi tuliwaumba watu baada ya Mūsā, wakakaa kwa muda mrefu, wakasahau ahadi ya Mwenyezi Mungu, wakaacha amri yake. Wala hukuwa ni miongoni mwa wakazi wa mji wa Madyan ukiwasomea kwao Kitabu chetu, na kwa hivyo ikakujia habari yao na ukaisimulia. Lakini habari uliokuja nayo kuhusu Mūsā ni wahyi na ni ushahidi wa utume wako.
Na hukuwako, ewe Mtume, upande wa jabali la Tūr tulipomuita Mūsā, na hukushuhudia lolote katika hayo. Lakini sisi tulikutumiliza ukiwa ni rehema kutoka kwa Mola wako, ili uwaonye watu ambao hawakujiwa na muonyaji kabla yako, huenda wao wakakumbuka wema uliokuja nao wakaufuata na uovu ulioukataza wakajiepusha nao.
Na lau si adhabu iteremke kwa hawa makafiri kwa sababu ya ukafiri wao, kisha waseme, «Si mwanzo utuletee Mtume kwetu, tupate kuzifuata aya zako zilizoteremshwa kwenye Kitabu chao na tuwe ni miongoni mwa wenye kukuamini»
Na alipowajia Muhammad watu hawa akiwa ni muonyaji kwao walisema, «Si apewe, huyu aliyetumilizwa kwetu, mfano wa kile alichopewa Mūsā, cha miujiza inayoonekana na Kitabu kilichoteremshwa mara moja.» Waambie, ewe Mtume, «Je, si Mayahudi walikikanusha kile alicholetewa Mūsā hapo kabla? Walisema kwamba ndani ya Taurati na Qur’ani kuna aina mbili za uchawi zilizosaidiana katika uchawi utokanao na hivyo viwili, na wakasema, «Sisi ni wenye kuvikanusha vyote viwili.»
Waambie hawa, ewe Mtume, «Basi Leteni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho ni cha sawa zaidi kuliko Taurati na Qur’ani, nipate kukifuata mkiwa nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»
Wasipokuitikia kwa kuleta Kitabu, na hawakusaliwa na hoja yoyote, basi ujue kwamba wao wanafuata matamanio yao. Na hakuna yoyote aliye mpotevu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake bila ya kuwa na uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Hawaafikii kuifikilia haki watu madhalimu walioenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na wakakiuka mipaka Yake.
Na kwa hakika, tuliifafanua na kuieleza Qur’ani kwa kuwaonea huruma watu wako, ewe Mtume, huenda wao wakakumbuka na wakawaidhika nayo.
Wale ambao tuliwapa Kitabu kabla ya Qur’ani, nao ni Mayahudi na Wanaswara ambao hawakugeuza, wanaiamini Qur’ani na wanamuamini Muhammad, rehema na amani zimshukiye.
Na pindi isomwapo hii Qur’ani kwa wale tuliowapa Kitabu wanasema, «Tumeiamini na tumeifuata kivitendo, hiyo ni haki itokayo kwa Mola wetu, hakika sisi tulikuwa, kabla haijateremka, ni Waislamu wenye kumpwekesha, kwani Dini ya Mwenyezi Mungu ni moja, nayo ni Uislamu.»
Hawa ambao sifa zao zimetangulia, watapewa malipo ya matendo yao mema mara mbili: ya kukiamini Kitabu chao na kuiamini kwao Qur’ani kwa vile walivyosubiri. Na miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao wanalikinga baya kwa zuri, na katika kile tunachowaruzuku wanatumia katika njia ya uzuri na wema.
Na wanaposikia, watu hawa, maneno ya ubatilifu, hawayapulikizi, na wanasema, «Sisi tuna matendo yetu tusiyoyaepuka, na nyinyi muna matendo yenu msiyoyaepuka. Sisi hatujishughulishi kuwarudi nyinyi, na hamtasikia kutoka kwetu isipokuwa mema, na hatutasema na nyinyi kulingana na ujinga wenu, kwa kuwa sisi hatutaki njia ya wajinga na hatuipendi.» Na haya ni miongoni mwa maneno mazuri zaidi ambayo walinganizi kwa Mwenyezi Mungu wanayasema.
Wewe, ewe Mtume, humuongoi, uongofu wa kumuafikia, unayependa aongoke. Lakini hilo liko kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu, Anamuongoa Anayemtaka kumuongoa kwenye Imani na kumuafikia aifuate. Na Yeye Ndiye Anayemjua zaidi anayefaa kuongoka, hivyo basi Anamuongoa.
Na makafiri wa Makkah wanasema, «Tukiifuata haki uliyotuletea na tukajiepusha na wategemewa na waungu, tutanyakuliwa kutoka kwenye ardhi yetu kwa kuuawa na kutekwa na kuporwa mali.» Kwani hatukuwafanya wao wamakinifu ndani ya mji wa amani, ambao ndani yake tumeharamisha umwagaji damu na ambao yanaletwa huko matunda ya kila aina yakiwa ni riziki kutoka kwetu? Lakini wengi wa hawa washirikina hawajui kadiri ya neema hizi kwao, wakapata kumshukuru Aliyewaneemesha wao kwazo na wakamtii.
Na wengi miongoni mwa watu wa miji tuliwaangamiza yalipowapumbaza wao maisha yao yakawashughulisha wasiwaamini Mitume, kwa hivyo wakakufuru na wakapita kiasi. Basi hayo ndio majumba yao, hayakukaliwa baada yao isipokuwa machache katika hayo. Na sisi daima ndio wenye kuwarithi waja: tunawafisha, kisha wanarejea kwetu tukawalipa kwa matendo yao.
Na hakuwa Mola wako, ewe Mtume, ni mwenye kuiangamiza miji iliyo pambizoni mwa Makkah katika zama zako mpaka Atumilize kwenye kilele cha miji hiyo, nacho ni Makkah, Mtume atakayewasomea wao aya zetu. Na hatukuwa ni wenye kuiangamiza miji isipokuwa na watu wake wanajidhulumu wenyewe kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumuasi, basi wao kwa hivyo wanastahili mateso na adhabu.
Na chochote kile mlichopewa, enyi watu, cha mali na watoto, basi hayo ni starehe ya nyinyi kustarehe nayo katika maisha haya ya kilimwengu na ni pambo la kujipamba nalo. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu, yaliyowekewa watu walio watiifu Kwake na wenye kumtegemea, ni bora zaidi na ni yenye kusalia zaidi, kwani hayo ni ya daima yasiyomalizika. Basi nyinyi hamuwi na akili, enyi watu, ya kuzingatia kwayo, mkajua lema na ovu?
Je, yule tuliyomuahidi Pepo, miongoni mwa viumbe wetu, kwa sababu ya kututii, akawa ni mwenye kupata alichoahidiwa na ni mwenye kukifikia, ni kama yule tuliyempa, katika uhai wa kilimwengu, starehe zake, naye akastarehe nazo na akaipa mbele ladha ya karibu kuliko ile ya baadaye, kisha yeye akawa ni mwenye kuhudhurishwa Siku ya Kiyama ili ahesabiwe na alipwe? Makundi mawili haya hayalingani. Basi mwenye akili ajichagulie nafsi yake kile kilicho bora kuchagua, nacho ni kule kumtii Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi Zake.
Na siku ambayo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atakapowaita wale waliomshirikisha Yeye wategemewa na masanamu ulimwenguni, awaambie, «Wako wapi washirika wangu ambao nyinyi mlikuwa mkidai kuwa wao ni washirika wangu?»
Watasema wale ambao imethibiti kwao adhabu, nao ni walinganizi wa ukafiri, «Mola wetu! Hawa ndio tuliowapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyopotea sisi. Tumejiepusha kwako na urafiki wao na uokoaji wao. Hawakuwa ni sisi wanaotuabudu, Hakika ni kwamba wao walikuwa wakiwaabudu mashetani.»
Na wataambiwa, Siku ya Kiyama, wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, «Waiteni washirika wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu.» Na wao wakawaita na wasiwajibu. Na wakaiona wazi adhabu, na lau wao wangalikuwa ni waongofu ulimwenguni, hawangaliadhibiwa.»
Na siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawaita hawa washirikina na aseme, «Mliwajibu vipi Mitume katika yale tuliyowatuma wao kwenu?»
Hapo hoja zao zote zitafichika, wasijue ni hoja ipi waitumie. Wao hawatoulizana wao kwa wao kuhusu hoja za kuzitumia, maswali yenye nafuu.
Ama yule aliyetubia kati ya washirikina na akamtakasia Mwenyezi Mungu ibada na akafanya matendo yanayoambatana na amri Yake na Mtume Wake, yeye ni katika wale wanaofuzu katika Nyumba Mbili.
Na Mola wako anaumba anachokitaka kukiumba, na anamteua awe karibu na Yeye Anayemtaka katika viumbe wake. Na hakuna yoyote mwenye chochote cha amri na uteuzi. Kwa hakika, hilo ni la Mwenyezi Mungu Peke Yake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ametukuka na kuepukana na ushirikina wao.
Na Mola wako anayajua yale yanayofichwa na vifua vya waja Wake na yale wanayoyafanya waziwazi.
Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Ambaye hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Ni Zake sifa njema na shukrani katika ulimwengu na Akhera. Na ni Wake uamuzi baina ya waja Wake. Na Kwake mutarudishwa baada ya kufa kwenu, muhesabiwe na mulipwe.
Sema, ewe Mtume, «Nipeni habari, enyi watu, iwapo Mwenyezi Mungu Angaliwaekea usiku wa daima mpaka Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu angaliwaletea mwangaza wa nyinyi kupata kuona? Basi kwani nyinyi hamsikii kwa namna ya kufahamu na kukubali?»
Waambie, «Nipeni habari iwapo Mwenyezi Mungu Angaliwaekea mchana wa daima mpaka Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu angaliwaletea usiku wa nyinyi kutulia na kupumzika ndani yake? Basi hamuoni kwa maangalizi yenu kule kupishana kwa usiku na mchana?»
Na miongoni mwa rehema Yake kwenu, enyi watu, ni kuwafanyia usiku na mchana Akatafautisha baina ya viwili hivi, Akaufanya huu usiku kuwa ni giza, ili mutulie humo na miili yenu ipumzike. Na Akawafanyia mchana kuwa ni mwangaza, ili mutafute maisha yenu na ili mumshukuru Yeye kwa kuwapa nyinyi neema zake hizo.
Na Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawaita hawa washirikina Awaambie, «Wako wapi washirika wangu ambao mulikuwa mukidai duniani kwamba wao ni washirika wangu?».
Na tutamtoa kwenye kila ummah, miongoni mwa ummah zenye kukanusha, shahidi, naye ni Nabii wao, atakayetoa ushahidi juu ya yaliyopita duniani ya ushirikina wao na ukanushaji wao Mitume wao. Tukaziambia ummah hizo zilizokanusha Mitume wake na yale waliyoyaleta kutoka kwa Mwenyezi Mungu, «Leteni hoja yenu juu ya kile mlichomshirikisha nacho Mwenyezi Mungu.» Wakati huo watajua kuwa hoja nzuri ni ya Mwenyezi Mungu juu yao, kuwa haki ni ya Mwenyezi Mungu, na kitawaondokea kile walichokuwa wakimzulia Mola wao kisiwanufaishe hiko, bali kiwadhuru na kiwafikishe kwenye Moto wa Jahanamu.
Hakika Qārūn alikuwa ni miongoni mwa watu wa jamii ya Mūsā, rehema na amani zimshukiye, akakiuka mpaka wake katika kuwa na kiburi na ujabari juu yao. Na tulimpa Qārūn mahazina mengi ya mali, mpaka ikafikia kiwango cha kuwa funguo zake zinawaelemea idadi kubwa ya watu wenye nguvu kuzibeba. Walipomuambia watu wake, «Usifanye kiburi ukawa na gogi la furaha kwa mali uliyonayo. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi kati ya waja wake wale wenye kiburi ambao hawamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kile Alichowapa.
«Na utafute, kwa mali Aliyokupa Mwenyezi Mungu, malipo mema ya Nyumba ya Akhera, kwa kufanyia mambo ya kumtii Mwenyezi Mungu duniani, na usiache fungu lako la duniani la kustarehe humo kwa halali bila kupita kiasi, na uwafanyie watu hisani kwa kuwapa sadaka kama vile Mwenyezi Mungu Alivyokufanyia hisani kwa kukupa mali mengi haya, na usitafute kile Alichokiharamisha Mwenyezi Mungu cha kuwadhulumu watu wako, kwani hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi waharibifu, na Atawalipa kwa matendo yao mabaya.»
Akasema Qārūn kuwaambia watu wake waliomuwaidhia, «Kwa hakika, mahazina haya ya mali nimeyapata kutokana na ujuzi na uwezo.»Kwani Qārūn hajui kwamba Mwenyezi Mungu ameshawaangamiza ummah wengi kabla yake yeye waliokuwa na nguvu zaidi za kushinda na ukusanyaji zaidi wa mali? Na hawataulizwa wahalifu kuhusu dhambi zao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Anazijua, isipokuwa wataulizwa maulizo ya kuwalaumu na kuwasimanga. Na Atawatesa Mwenyezi Mungu kulingana na ujuzi Wake kuhusu wao.
Basi akatoka Qārūn akiwa kwenye pambo lake, akitaka kwa kufanya hivyo kuonyesha ukubwa wake na wingi wa mali yake. Na walipomuona wale wanaotaka pambo la uhai wa kilimwengu walisema, «Tunatamani lau sisi tungalipatiwa mfano wa kile alichopatiwa Qārūn, cha mali, pambo na heshima. Kwa kweli, Qārūn ni mwenye sehemu kubwa ya dunia.»
Na wakasema, wale waliopewa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na Sheria Yake na wakijua uhakika wa mambo, kuwaambia wale waliosema, «Tunatamani tuwe na mfano wa kile alichopatiwa Qārūn», «Ole wenu! Muogopeni Mwenyezi Mungu na mumtii. Malipo mema ya Mwenyezi Mungu ni bora, kwa aliyemuamini Yeye na Mitume Wake na akafanya matendo mema, kuliko kile alichopatiwa Qārūn. Na haupokei ushauri huu na akaafikiwa kuufuata na kuufanyia kazi isipokua yule anayepigana jihadi na nafsi yake, anayevumilia katika kumtii Mola wake na anayejiepusha na mambo ya kumuasi.
Basi tukamdidimiza Qārūn pamoja na nyumba yake ndani ya ardhi. Na hakuwa na askari wa kumuokoa badala ya Mwenyezi Mungu, na hakuwa ni mwenye kujikinga na Mwenyezi Mungu yatakapomshukia mateso Yake.
Na wale waliotamani kuwa kama yeye jana yake wakawa wanasema, wakiwa na uchungu, wenye kuzingatia na wenye kuiogopa adhabu isiwashukie, «Hakika Mwenyezi Mungu Anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake, na Anambania Anayemtaka miongoni mwao. Lau si Mwenyezi Mungu kutuneemesha kwa kutotuadhibu kwa tulilolisema, Angalitudidimiza sisi ardhini kama Alivyomfanya Fir’awn. Kwani hujui kwamba makafiri hawafaulu, hapa duniani wala Akhera?
Hiyo ndiyo Nyumba ya Akhera. Tumewapatia, ile starehe yake, wale ambao hawataki kuifanyia kiburi haki hapa duniani wala kufanya uharibifu humo. Na mwisho wenye kushukuriwa, nayo ni pepo, ni wa yule aliyejikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu na akafanya mema na akaacha mambo yaliyoharamishwa.
Mwenye kuja, Siku ya Kiyama, na utakasaji wa Mwenyezi Mungu Mmoja na matendo mema yanayolingana na Sheria ya Mwenyezi Mungu, basi yeye atakuwa na malipo makubwa yenye kheri zaidi kuliko kile alichokifanya. Na kheri hiyo ni Pepo na starehe ya daima. Na mwenye kuja na matendo mabaya, hawatalipwa hao waliofanya maovu kwa matendo yao, isipokuwa yale waliokuwa wakiyafanya.
Hakika Yule Aliyekuteremshia wewe, Qur’ani, ewe Mtume, na akakulazimisha wewe uifikishe na ushikamane nayo, ni Mwenye kukurudisha kule ulikotoka, nako ni Makkah. Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mola wangu Anamjua zaidi yule aliyeleta uongofu na yule ambaye ameenda nje ya haki waziwazi.»
Na hukuwa ukitarajia, ewe Mtume, kuteremkiwa na Qur’ani, lakini Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Alikurehemu Akakuteremshia. Basi mshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema Zake, na usiwe ni mwenye kuwasaidia watu wa ushirikina na upotevu.
Na wasikuepushe wewe washirikina hawa na ufikishaji aya za Mola wako na hoja Zake baada ya kuwa Amekuteremshia kwako, na ufikishe ujumbe wa Mola wako, na usiwe ni miongoni mwa washirikina katika kitu chochote.
Wala usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa mwingine. Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kila kitu ni chenye kuangamia na kutoeka isipokuwa uso Wake. Uamuzi ni Wake. Na Kwake Yeye mutarudishwa baada ya kufa kwenu ili muhesabiwe na mulipwe. Katika aya hii kuna kuthibitisha sifa ya uso wa Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, kama inavyonasibiana na ukamilifu Wake, ukubwa Wake na utukufu Wake.